**********************
Na. INSP FRANK LUKWARO
Timu ya mpira wa miguu ya Polisi Tanzania inayoshiriki ligi kuu ya NBC imeingia makubalinao ya udhamini wa maji ya kunywa na Nabii Clear Malisa wa Kanisa la Heaven of Peace Kingdom Embassy.
Mkataba huo ambao ni wa kipindi cha mwaka mmoja ukiwa na thamani ya Shilingi Milioni 50 ambapo pia udhamini huo utajikita katika kuboresha Idara ya Habari na Mawasiliano katika kuwafikia mashabiki wake kupitia mitandao ya kijamii.
Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu wa Klabu hiyo Michael Mtebene amesema udhamini huo utasaidia kwa kiasi kikubwa timu hiyo kufanya vizuri kwa sababu wachezaji watapata huduma ya maji bila ukwamo wa aina yeyote na kazi yao itakuwa ni kucheza na kuwafurahisha mashabiki ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kwa Upande wake Nabii Clear Malisa amesema ameamua kuidhamini timu hiyo kwa kuwa ni timu ambayo imekuwa ikifanya vizuri na ina malengo ya kufanya vizuri katika ligi ya NBC.
Nabii Malisa alisema Polisi na jamii ni marafiki hivyo katika kukuza ushirikiano huo ameona ni vyema kuisaidia klabu hiyo ili iendelee kuinua maisha ya vijana wanaocheza katika timu hiyo.
Naye Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa timu Inspekta Frank Lukwaro amezionya timu watakazokutana nazo katika michezo inayofuata kujipanga kwa kuwa hivi sasa wanakuja kivingine baada ya kupata udhamini huo.
Alisema pamoja na maji lakini pia watakuwa wakiwekwa katika maombi ili waweze kufanya vizuri katika ligi hyo ambayo inaendelea katika viwanja mbalimbali hapa nchini.
“Wapinzani wetu wajipange, kama mnavyotujua sisi ndio wafunga buti halisi sasa kwa udhamini huu tunakwenda kujiimarisha zaidi na kutufanya vizuri katika ligi ya msimu huu japokuwa ligi ni ngumu lakini Polisi hatujawahi kushindwa na tutapambana mpaka tone la mwisho la damu”Alisema Lukwaro