KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Francis Michael,akizungumza wakati akifungua kikao kazi cha kufanya tathimini ya utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa elimu Jumuishi Tanzania wa mwaka mmoja 2021/22 kilichofanyika leo Oktoba 4,2022 jijini Dodoma.
SEHEMU ya washiriki wakifatilia hotuba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Francis Michael, wakati akifungua kikao kazi cha kufanya tathimini ya utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa elimu Jumuishi Tanzania wa mwaka mmoja 2021/22 kilichofanyika leo Oktoba 4,2022 jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Elimu Maalum, Dk Magreth Matonya,akizungumza wakati wa kikao kazi cha kufanya tathimini ya utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa elimu Jumuishi Tanzania wa mwaka mmoja 2021/22 kilichofanyika leo Oktoba 4,2022 jijini Dodoma.
KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Francis Michael,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua kikao kazi cha kufanya tathimini ya utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa elimu Jumuishi Tanzania wa mwaka mmoja 2021/22 kilichofanyika leo Oktoba 4,2022 jijini Dodoma.
…………………………………….
Na Alex Sonna-DODOMA
KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Francis Michael,amewataka wadau wa elimu jumuishi nchini kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora unazingatia ujumuishi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Hayo ameyasema leo Oktoba 4,2022 jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha kufanya tathimini ya utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa elimu Jumuishi Tanzania wa mwaka mmoja 2021/22.
Amesema kuwa kipaumbele kiwekwe katika uboreshaji wa mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji hususani kwenye shule, vyuo vya ualimu, vyuo vya maendeleo ya wananchi, vyuo vya ufundi stadi na vikuu.
“Nitoe rai kwa viongozi wa taasisi zinazojihusisha na utoaji elimu jumuishi, ziendelee kushirikiana na serikali kuhamasisha umuhimu wa elimu kwa watu wenye mahitaji maalum,”amesema Dk.Michael
Aidha Dk.Michael amesema kuwa kuna umuhimu wa kuchangia juhudi za serikali katika kuwapatia huduma stahiki wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika ujifunzaji na kutimiza ndoto zao.
Amesema kuwa lengo la kikao hicho ni kupata uelewa kuhusu mkakati wa Taifa wa Elimu Jumuishi wa mwaka 2021/22-2025/26, kufanya mawasilisho ya serikali na wadau kuhusu utekelezaji wa mkakati huo na kufanya tathimini kwa mwaka wa kwanza.
“Kikao hiki ni muhimu kujadili namna ya kuboresha utoaji elimu Jumuishi nchini kwa kufanya tathimini ya utekelezaji na kubaini changamoto mbalimbali ili kutoa huduma bora kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum,”ameeleza
Awali Mkurugenzi wa Elimu Maalum, Dk Magreth Matonya amesema kuwa kupitia kikao hicho kutakuwa na upokeaji maoni kuhusu namna ya kuboresha sera na mitaala ya elimu ili kundi hilo lihusishwe ndani yake.