********
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
KLABU ya Yanga imeendelea kutoa matokeo mazuri kwenye ligi ya NBC baada ya leo kuibuka mshindi na kujinyakulia pointi tatu dhidi ya Ruvu Shooting, mechi ambayo imepigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Ruvu Shooting walicheza kandanda murua kwenye mchezo huo katika kipindi cha kwanza licha ya kutengeneza nafasi kadhaa na kushindwa kuzitumia vizuri na kufanya matokeo kuwa 0-0 kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili Yanga iliingia ikiwa imeimarika kwani walibadika kwa kiasi kikubwa na kufanikiwa kupata bao la kwanza kupitia kwa Feisal Salum ambaye alipata bao akipokea krosi nzuri kutoka kwa Joyce Lomalisa.
Bao la pili la Yanga Sc liliwekwa kimyani na nahodha wao Bakari Mwamnyeto ambaye ni goli lake la pili kwa msimu huu 2022/2023.