**************
Na Mwandishi wetu, Morogoro
UMOJA wa Waandishi wa Habari Wanawake mkoa wa Dar es Salaam, kupitia Asasi ya Sauti ya Matumaini (SAMAF) kwa kushirikiana na Kampuni ya Simu ya Itel, umetoa msaada wa chakula na taulo za kike kwa watoto wenye ulemavu wanaoishi katika mazingira magumu wa Kituo cha Amani na Mihayo vilivyopo kata ya chamwino Mkoani Morogoro.
Akizungumza wakati wa kutoa msaada huo, Mwanzilishi wa umoja huo, Penina Malundo, alisema taasisi yao inaendelea kuhakikisha inarudisha tabasamu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na wale wenye ulemavu kwa kuwasaidia vitu mbalimbali pamoja na kuwapa elimu ya afya, kujitambua pamoja na masuala ya ukatili wa kijinsia.
Alisema wamekuwa wakitoa taulo la kike kwa mabinti wenye ulemavu ili kuwasaidia mabinti hao kupata hedhi salama ambayo itawafanya kutokuwa wanyonge kwa kuendelea na shughuli zao ikiwamo masomo.
“Hii sasa ni awamu ya tatu kwa mwezi huu wa tisa kutoa elimu ya afya ya uzazi, kujitambua na ukatili wa kijinsia tumeweza kufikia shule tatu ambazo ni shule ya msingi Buguruni Viziwi, Maweni, Kigamboni, Vijibweni na Kituo cha Amani na Mihayo mkoani Morogoro jumla ya mabinti 200 tumewafikia kna kampeni yetu ya ‘ithamini na ilinde kesho yangu’,” alisema na kuongeza;
“Mkoani Morogoro tumeweza kushirikiana na Kampuni ya Simu ya Itel katika kufanikisha shughuli hii na wadau wengine ikiwamo Shree Jalalam katika kuwasaidia mahitaji mbalimbali na kuwarudisha katika furaha makundi hayo.”
Alitaja vitu walivyowakabidhi watoto hao ni pamoja na mchele,unga ,mafuta ya kula,maharage,taulo za kike sabuni ya unga, maji, juisi ja biskuti ambazo zimetolewa na wadau hao ikiwa na lengo la kuisaidia SAMAF kufikia watoto waliokatika mazingira magumu.
Aliitaka jamii kuendelea kuwatunza watoto hao na kuwaona nao wana haki kama wengine ili kurudisha tabasamu kwao.
Kwa Upande wake, Meneja uhusiano wa Kampuni ya Itel, Fernando Mfuole, alisema kampuni yao ya Itel inaendesha kampeni ya kurudisha fadhira kwa jamii katika kila kila faida wanayopata katika Shule mbalimbali au katika vituo vya watoto vya kulelea yatima,wanaoishi mazingira magumu au venye watoto wenye ulemavu.
“Tunafanya hivi katika mikoa yote mahali popote nchini, tunarudisha fadhila kwa jamii hii ni kuhakikisha tunawasaidia watoto waliopo katika makundi haya leo tumeweza kutoa mahitaji mbalimbali yanayohitajika ili kuweza kurudisha furaha za watoto hawa wa kituo cha Amani na Mihayo mkoani Morogoro,”alisema.
Alisema Itel imeweza kuguswa na kuhakikisha inawafikia katika kuwapatia kile kitu walichobarikiwa katika faida wanayoipata kwenye bidhaa zake.
Naye Msimamizi wa kituo cha Amani, Padri Beatus Msewando, aliishukuru Kampuni ya Itel na SAMAF kwa msaada huo na kuiomba jamii kujitokeza kusaidia kituo hicho kwa sababu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kutokana na wingi wa watoto wanaowapokea.
“Katika huduma zetu hizi tunaona wengine wanaletwa hawana ndugu wala pakukaa,kwa hiyo tunawasaidia kuishi nao huku tukiwafundisha mambo mbalimbali kama kazi za mikono,ikiwamo kilimo na uvuvi ili kuwapa nyenzo za kuja kujitegemea,”alisema
Mwisho