Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akifungua kikao cha wadau wa mazingira kilichojadili mikakati ya upatikanaji fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kikao hicho cha siku nne kinafanyika jijini Arusha.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akifuatilia mawasilisho katika kikao kazi cha wadau wa mazingira kinachofanyika kwa siku nne katika Hotel ya Kibo Palace Arusha. Wengine katika picha (kutoka kushoto) Dkt. Omar Shajak Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais – Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Bw. Abdallah Mitawi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua kikao cha wadau wa mazingira kilichojadili mikakati ya upatikanaji fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kikao hicho cha siku nne kinafanyika jijini Arusha.
…………………………….
SERIKALI imesema takribani dola Bilioni 19.2 za kimarekani zitatumika katika kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kukabiliana na mabadiliko tabianchi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt.Selemani Saidi Jafo amesema hayo leo 03/10/2022 katika kikao cha wadau wa Mazingira kinachofanyika Jijini Arusha kwa muda wasiku nne kujadili Mikakati ya nchi kuongeza uwezo wa kupata fedha za kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.
Amesema Serikali inachukua hatua kubwa kama vile kuandaa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi 2021, Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022 – 2023) na Miongozo na Kanuni za Biashara ya Kaboni, ikiwa ni jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.
“Tanzania pia imetekeleza miradi mbalimbali ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kuta katika fukwe Mkoani Mtwara na Visiwani Zanzibar pamoja na miradi mingine katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, nishati, misitu, viwanda, TEHAMA pamoja na kujenga uwezo wa kitaasisi” Alisisitiza Dkt. Jafo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt. Omar Shajak amesema kwa upande wa Zanzibar kikao kazi hiki pia kitaweka mikakati ya kupata fedha zitakazotumika pande zote mbili za Muungano
Nae Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Andrew Komba amesema kwa muda wa siku nne Mashirika ya Kitaifa, Asasi za Kiraia na taasisi za kifedha pamoja na mambo mengine watapitia msimamo wa Tanzania kuelekea Mkutano wa 27 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi utakaofanyika tarehe 6 – 18 Novemba 2022, Sharma el-Sheikh, Misri.