Mkuu wa wilaya ya Arusha ,Said Mtanda akizungumza wakati akiomba kura jana
Mwenyekiti wa ccm wilaya ya Arusha mjini Dk Willfred Soillel akizungumza kwenye mkutano huo jijini Arusha mara baada ya kuibuka mshindi .
***********************
Julieth Laizer, Arusha.
Arusha.Mkuu wa wilaya ya Arusha, Said Mtanda ameondoa aibu baada ya wajumbe kumpa ridhaa ya kuwa miongoni mwa wajumbe wa mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa kutokea Arusha.
Mtanda aliomba kura jana kwa staili ya kipekee mbele ya wajumbe ambapo alijinasibu kuwa wajumbe wamchague ili wanahabari wakose stori ya kuandika kuwa kaangukia pua.
“naomba kura zenu ili waandishi wakose cha kuandika kuwa Dc apigwa chini na wajumbe,nimefanya kazi nyingi na nyie ni mashahidi ukinibiipu nakupigia,ukinitumia meseji nakujibu sasa ni zamu yenu kunifuta aibu hii kwa wanahabari” amesema Mtanda.
Baada ya kujieleza hivyo wajumbe walianguka kicheko na hatimaye kumchagua yeye Mtanda,Violet Mfuko na Yusuf Khatry kuwa wajumbe wa mkutano mkuu Taifa.
Wakati huo huo mkutano huo ulimpa ridhaa Dk Willfred Soillel kuwa Mwenyekiti wa ccm wilaya ya Arusha kwa kumchagua kwa kura 315 huku akiwaacha kwa mbali wapinzani wake .
Wengine waliowania nafasi hiyo ni pamoja na aliyewahi kuwa mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Arusha, Saipulan Ramsey aliyepata kura 155 , mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wilaya ya Arusha ( UWT)Mwinyimvua kura 135 na Mwenyekiti wa ccm kata ya Osunyai ,Elirehema Nnko aliyeambulia kura 15.
Dkt Soillel amewahi kuwa mwenyekiti wa Ccm wilaya ya Arusha na hivyo sasa hivi amerudi kwa mara ya pili tena kwa nafasi hiyo ya mwenyekiti.
Soillel amewashukuru wajumbe kwa kumrejesha madarakani akiahidi uongozi uliotukuka na kuwaomba wanaccm wampe ushirikiano ili kuendelea kuimarisha chama.
Aidha wajumbe pia walimchagua Antony Maswi kuwa katibu mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Wilaya ya Arusha akifanikiwa kutetea nafasi yake kwa kura 95.
Wakati huo huo Noel Severe alichaguliwa kwa kishindo kwa kupata kura 438 na kuwa mwenyekiti mpya wa ccm wilaya ya Arumeru na kumwangusha mwenyekiti wa siku nyingi Simon Saning’o aliyeambulia kura 262.