******************
Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa uchaguzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wamembariki tena Alhaj AbdulSharifu Zahoro kuwa Mwenyekiti wa chama hicho kwa kipindi cha mwaka 2022-2027
Uchaguzi huo ulikuwa na wajumbe zaidi ya 1,500 kati ya hao wajumbe 901 walimchagua Sharifu kati ya kura 1,487 zilizopigwa sawa na asilimia 60.5.
Mgombea huyo aliwashinda wagombea wenzake Alhaj Amiry Mkang’ata aliyepata kura 524 sawa na asilimia 55.2 na kufuatiwa na Joyce Emmanuel kura 62 asilimia 4.1.
Akitangaza matokeo alhaj Abdallah Sakasa aliwatangaza wagombea walioshinda kwenye nafasi mbalimbali, katika uchaguzi huo uliokuwa chini ya Mwenyekiti wa muda, Ridhiwani Kikwete akisaidiana na Katibu wa CCM Bagamoyo Yusufu Ramadhani.
Zainabu Abdallah Mkuu wa Wilaya hiyo, Yusufu Kikwete na Debora Rashid walichaguliwa kuwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu CCM Taifa.
Nae Ridhiwani alieleza ,kuchaguliwa kwa Sharifu kumeonesha ni namna gani wanaCCM hao walivyoridhishwa na uongozi wake katika kipindi alichokiongoza chama hicho.
Akitoa shukran zake kwa wajumbe ,Sharifu aliwaomba wanachama hao kuvunja makundi na kuwa kitu kimoja na kwamba ndani ya CCM hakuna mshindi.
“Niwashukuru wajumbe wote pamoja na meza kuu kwa kusimamia zoezi hili, niwaombe wanachama wenzangu kwamba makundi yamevunjwa, twendeni tukakijenge chama chetu,” alisisitiza Sharifu.