*********************
Na Mwandishi wetu, Arusha
TAASISI ya wanahabari wa kusaidia jamii za Pembezoni (MAIPAC) inatarajiwa kuwa na mashirikiano na taasisi zisizo za kiserikali za nchini CANADA ili kuwajengea uwezo wanahabari na kusaidia jamii ya pembezoni.
Mkurugenzi wa shirika la MAIPAC, Mussa Juma ametoa taarifa jana katika hafla ya kumuaga mshauri elekezi wa MAIPAC kutoka nchini Canada, Lori Leugalt ambaye alikuwa nchini kulijengea uwezo shirika la MAIPAC.
Juma amesema licha ya mshauri huyo kutoa mafunzo kwa MAIPAC jinsi ya kuandaa miradi na kutafuta wafadhili walifikia makubaliano ya kuwa na mahusiano na mashirika ya Canada ambayo yanajihusisha na kusaidia jamii za pembezoni na wanahabari.
Amesema mtaalam huyo ambaye ameletwa nchini maalum kusaidia MAIPAC na taasisi ya CESO kwa ushirikiano na ubalozi wa Canada ujio wake umekuwa na mafanikio makubwa.
Awali Legault amesema anashukuru kuja nchini Tanzania na kufanyakazi na MAIPAC kwani pia amejifunza utekelezwaji miradi ya MAIPAC .
Amesema amejionea kazi za mradi wa uhifadhi mazingira,vyanzo vya maji na misitu kwa maarifa asilia ambao unafadhiliwa na shirika la maendeleo la umoja wa Mataifa (UNDP) na kusimamiwa na jumuiko la maliasili Tanzania (TNRF).
“Nimefurahi kuwa Tanzania na MAIPAC watu wa Tanzania ni wakarimu sana na tutaendelea kushirikiana,” amesema.
Afisa Miradi wa MAIPAC Debora Makando amesema wamejifunza mengi kutoka kwa mfadhili huyo.
Makando amesema kutokana na mafunzo waliyopata wataboresha utendaji wa kazi wa MAIPAC.
Afisa Tawala wa MAIPAC Andrea Ngobole amesema wanahabari na jamii za pembezoni zitanufaika na mahusiano ya MAIPAC na Taasisi za Canada na CESO.
“Tunataraji kuwa na miradi ya kubadilishana uzoefu kusaidia jamii za pembezo na athari za mabadiliko ya tabia nchi,” amesema Ngobole.