**********************
Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
SERIKALI inakwenda kuanzisha mradi mkubwa wa jiji la kibiashara (Kwala International Commercial City) linakalo fungua milango ya kibiashara na uchumi na inategemewa kuwa kubwa ndani ya Afrika.
Aidha Utekelezaji wa ujenzi wa kazi zote kwa awamu za sasa katika Bandari kavu Kwala, Kibaha Vijijini umefikia asilimia 69 huku Bandari kavu ikiwa imefikia asilimia 72 ambapo inatarajia kushusha makontena 3,500 kwa wakati mmoja.
Mkuu wa wilaya ya Kibaha (Kamisaa),Sara Msafiri aliyaeleza hayo wakati akielezea utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa Kitaifa, Bandari kavu kwala , ikiwa ni sehemu ya taarifa ya Serikali Kibaha ,utekelezaji wa ilani ya CCM, katika mkutano mkuu wa chama cha Mapinduzi CCM Kibaha Vijijini.
Msafiri alisema , Mradi huo mkubwa ni mpango wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambao kwasasa upo kwenye hatua ya maandiko na kuandaa michoro.
Alisema , Mradi huo utagharimu mabilioni ya fedha na ukikamilika utashinda jiji la Dar es Salaam.
Msafiri alifafanua, mradi utachukua hekta 13 kwenye vijiji 30 upande wa Kisarawe kidogo na Chalinze na Kibaha Vijijini, na wananchi watakaochukuliwa ardhi yao watalipwa fidia.
“Niwaondoe hofu wananchi watakaochukukuliwa ardhi yao, watalipwa fidia na ardhi yao itapanda thamani, Hivyo waondokane na upotoshaji kuwa wanataka waondolewe kiholela”alieleza Msafiri.
Hata hivyo Kamisaa huyo alisema , eneo hilo pia litakuza uchumi, kwa kupita reli ya kisasa (SGR) ,na unatarajiwa kujengwa barabara ya mwendokasi ili kuinua pato la Taifa, kuongeza ajira .
Sambamba na Hilo, Kuna kongani iliyopo Disunyara yenye hekari 1,000 na sinotan iliyopo Kwala yenye hekari 2,500 ambazo zinakwenda kukuza sekta ya uwekezaji na viwanda.
Katika hatua nyingine alieleza, Utekelezaji wa ilani,kwa uwezeshaji wa mikopo ya vijana, wanawake na walemavu mikopo imeweza kutolewa ya kiasi cha sh. milioni 720.
Msafiri alifafanua, Serikali imetoa fedha za Uviko19 na kujenga vituo vya afya, madarasa na fedha za tozo kwa ajili ya uboreshaji miundombinu ya barabara.
Nae Meneja msimamizi wa mradi wa Mamlaka ya usimamizi wa bandari Tanzania , Alexander Ndibalema alieleza kwamba , ujenzi wa bandari kavu mkandarasi anaendelea na kazi na ujenzi wa kazi ya sasa unatarajia kugharimu zaidi ya sh.Bilioni 83.246 .
“Kwa upande wa ujenzi wa barabara ya zege Vigwaza-Kwala utaanza kutumika octoba mwaka huu .”
Ndibalema alieleza, gharama za uendelezaji wa Bandari hiyo katika awamu hii upande wa kusafisha eneo na ujenzi wa ukuta Bilioni 9.4 ,reli mchepuko km 1.3 milioni 677.328 na barabara km.15.5 kiwango cha Zege Bilioni Zaidi ya 36.
Alisema Jiji la Dar es Salaam limezidiwa kwa msongamano wa maroli hivyo Serikali ilielekeza kutafutwa eneo la kujengwa bandari hiyo na matunda sasa yanaonekana ili kupunguza msongamano wa magari.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Kibaha Vijijini, Safina Nchimbi alieleza, Kuna Jumla ya wanachama wapya 16,956 ,waliosajiliwa katika mfumo 14,133 waliolipa Ada ni 12,000.
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Michael Mwakamo aliwataka wananchi wa eneo litakalojengwa mradi wa jiji la Kibiashara kutunza maeneo Yao na kuacha kuyauza kwa hasara .