Biashara kati ya Tanzania na Nigeria imeongezeka kutoka shilingi bilioni 23 mwaka 2020 hadi shilingi bilioni 24 mwaka 2021.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb.) alipokuwa akishiriki katika hafla ya maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Nigeria yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam
Balozi Mulamula ameongeza kuwa takwimu za biashara na uwekezaji zinatia moyo kuona kiwango cha biashara kati ya nchi zetu mbili kimeendelea kuongezeka, kutoka shilingi bilioni 23 mwaka 2020 hadi shilingi bilioni 24 mwaka 2021. Kuhusu uwekezaji, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili Kampuni 23 za Nigeria ambazo zimewekeza Tanzania kwa uwekezaji wa jumla ya Dola za Kimarekani milioni 466.50 na kutoa takriban ajira 1,734.
“Nangependa kutumia fursa hii kuhimiza jumuiya zetu za wafanyabiashara kuangalia fursa za biashara zinazopatikana katika nchi hizi mbili (Tanzania na Nigeria). Serikali ya Tanzania imefungua milango yake kwa mtu yeyote karibuni kuwekeza,” amesema Balozi Mulamula
Tanzania na Nigeria zinashirikiana kwa karibu kukuza Ajenda ya mwaka 2030 ya Umoja wa Afrika. Hii inalazimu, miongoni mwa mambo mengine, kukuzwa kwa jamii zenye amani, usawa, na ajenda ya maendeleo ya bara la Afrika na watu wake.
Kwa Upande wake Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takalmawa amesema kuwa Nigeria inajivunia kuwa rafiki wa Tanzania kwani mataifa haya yamekuwa yakishirikiana kijamii katika masuala ya utamaduni, muziki, nyimbo na tamthilia….n.k
“Ushirikiano na umoja baina ya Nigeria na Tanzania umekuwa na misingi imara ya kukuza na kuimarisha diplomasia baina ya mataifa yetu mawili,” amesema Balozi Takalmawa
Balozi Takalmawa ameongeza kuwa biashara kati ya Nigeria na Tanzania imeongezeka ikilinganishwa na miaka iliyopita, kadhalika uwekezaji nao umeongezaka jambo ambalo linaashiria mazingira bora ya biashara na uwekezaji. Mbali na kuadhimisha siku ya Uhuru wa Nigeria, pia Waziri Mulamula alizindua maktaba katika ofisi za Ubalozi wa Nigeria hapa nchini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akisalimiana na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takalmawa katika Ofisi za Ubalozi wa Nigeria Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwasilisha hotuba yake wakati wa maadhimisho ya maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Nigeria yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamoja na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takalmawa wakikata utepe wa kufungua maktaba ya ubalozi wa Nigeria katika Ofisi za ubalozi huo Jijini Dar es Salaam
Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takalmawa akikabidhi nakala ya kitabu kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula baada ya kufungua maktaba ya ubalozi huo Jijini Dar es Salaam
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na baadhi ya mabalozi walioshiriki katika maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Nigeria yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam