Badhi ya wajumbe wa Mkutano mkuu wa CCM Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara wakiwa tayari kwenye uchaguzi wa CCM Wilaya hiyo unaotarajiwa kufanyika kesho jumapili Oktoba 2.
……………………….
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
KATIBU wa CCM wilaya ya Simanjiro, Mkoani Manyara, Amos Shimba (Shimba wa Shimba mwana Shimba) amesema wamejipanga kikamilifu ili kufanikisha uchaguzi wa kugombea nafasi mbalimbali za wilaya hiyo unatarajiwa kufanyika kesho jumapili Oktoba 2 mwaka huu kuanzia saa 4 asubuhi.
Shimba amesema wamejipanga kikamilifu ili kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika ipasavyo kwenye ukumbi wa shule ya sekondari Simanjiro kesho jumapili.
“Baadhi ya nafasi zitakazogombewa ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya, katibu mwenezi wa wilaya, wajumbe watatu wa mkutano mkuu wa Taifa na wajumbe wa mkoa na wilaya,” amesema Shimba.
Amesema Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imerudisha majina matatu ya Haiyo Mamasita, Kiria Laizer na Anna Shinini ili wagombee nafasi ya Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Simanjiro.
Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Manyara, Kiria Laizer amesema endapo akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM wilaya ataunganisha Simanjiro iwe moja katika kufanikisha maendeleo kupitia wanachama, chama na serikali.
Mgombea mwingine Anna Shinini amesema endapo atachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro ataondoa makundi na siasa za makambi ambayo yamekithiri Simanjiro.
Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wilaya ya Simanjiro, Haiyo Mamasita amesema endapo atachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, ndiyo ataamua ataachia nafasi gani kati ya hizo mbili endapo akishinda.
Mfanyabiashara maarufu Daniel Materi amesema anaomba wajumbe wamchague tena kwenye nafasi moja kati ya tatu za mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa.