Na Shamimu Nyaki, Dodoma
Ujenzi wa Jengo la Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Mji wa Serikali Mtumba Dodoma, umefika asilimia 50 na kutumia takriban Bilioni Saba mpaka sasa.
Kaimu Katibu Mkuu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Saidi Yakubu amesema hayo, katika mahojiano na Kipindi Cha Clouds 360 kutoka Clouds Media leo Septemba 30, Dodoma.
Eneo letu Lina ekari 7, na Jengo hili linalojengwa hapa litakua na ghorofa 6 ambazo zitajumuisha Ofisi za Idara na Vitengo, ofisi za viongozi, Kumbi za Mikutano pamoja na maeneo ya bustani na viwanja vidogo vya michezo” amesema Kaimu Katibu Mkuu Yakubu.
Ameongeza kuwa, Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan inatoa fedha kwa wakati kwa Mkandarasi ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kulingana na Mkataba.
Kwa upande wake Mkandarasi msimamizi wa Jengo hilo Bw. Omari Chitawala amesema ujenzi unazingatia masharti yote ya Mkataba ikiwemo ubora na viwango vinavyotambulika.
Aidha, Watangazaji hao walijionea ujenzi ukiendelea katika maeneo kadhaa ikiwemo umaliziaji wa ghorofa ya sita na uwekaji wa plasta katika ghorofa za chini za jengo hilo linalotarajiwa kugharimu takriban shilingi bilioni 22.7.
Ujenzi huo ulioanza Oktoba 2021 unatarajiwa kukamilika Oktoba 2023.