Na Mary Gwera, Mahakama
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amezindua rasmi Tovuti ya Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi (labourcourt.judiciary.go.tz) huku akizitaka Mahakama nyingine anazozisimamia kubuni njia mbalimbali zilizopo ndani ya uwezo wao ili kuweza kufikisha taarifa za kimahakama kwa wananchi wengi kwa urahisi zaidi.
Akizungumza leo tarehe 30 Septemba, 2022 katika hafla fupi ya kuzindua Tovuti ya Divisheni hiyo iliyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, Mhe. Siyani amesema kwa kuwa sera ya Mahakama inaelekeza kuimarisha matumizi ya TEHAMA kote nchini, hivyo ni muhimu kuendelea kuchukua hatua kadhaa ili kutimiza azma ya Mahakama ya kuwa na matumizi kamili ya mtandao ‘e-Judiciary’ ifikapo mwaka 2025.
“Kila Mahakama kote nchini ni vyema sana ikatafuta na kubuni namna tofautitofauti kulingana na uwezo wake kuona inawezaje kuwafikia wananchi walio wengi, hilo ndio lengo letu kusogeza huduma kwa wananchi, kwahiyo tovuti hii ni moja ya njia za kuwafikia wananchi, hivyo mwananchi yeyote mwenye simu janja popote alipo anaweza kupata taarifa kuhusu Mahakama hii” amesema Jaji Kiongozi.
Ameipongeza Divisheni ya Kazi kwa kuamua kutekeleza kwa vitendo ajenda ya uboreshaji wa huduma za Mahakama na mageuzi yaliyoainishwa katika Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021-2024/2025 unaolenga kuifanya Mahakama ya Tanzania kuwa Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’. Akiongeza kuwa, upatikanaji wa tovuti hiyo ni muhimu na una faida kubwa kwani itawawezesha Wadau wa Divisheni hiyo kuifikia Mahakama kwa urahisi zaidi.
Aidha; Mhe. Siyani amewasisitiza Viongozi wa Divisheni hiyo kuzingatia matumizi ya Kiswahili katika Tovuti ili wananchi wa aina zote waweze kupata taarifa zilizomo.
“Jambo jingine ambalo ningependa kusema kupitia hafla hii ni kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili kupitia tovuti. Kwa ngazi ya Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi imekuwa kinara na kuenzi matumizi ya lugha hii adhimu, hivyo, ni matarajio yangu na bila shaka nimefurahi kusikia kwamba, hatua zinachukuliwa kuhakikisha kuwa, tovuti hii inamuwezesha mwananchi kupata taarifa zote muhimu kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza,” amesisitiza Jaji Kiongozi.
Ameongeza kwa kuwaomba Wadau wa Divisheni hiyo hususani Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) hapa nchini kuendelea kushirikiana na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kutafsiri nyaraka mbalimbali za kimahakama zilizo katika lugha ya Kiingereza ikiwezo uamuzi na mikataba mbalimbali ya kimataifa kwenda kwenye lugha ya Kiswahili, lakini pia na kuanza kuweka misamiati mingi inayotumika katika Mahakama hiyo.
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi amesema lengo la kuanzisha tovuti ya Divisheni hiyo ni kuwarahisishia wadau wa Mahakama hiyo kupata kwa urahisi na kwa haraka taarifa mbalimbali ikiwemo rejea za Sheria na Kanuni za Kazi na Ajira, uamuzi wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani yanayohusisha mashauri ya kazi.
“Tovuti hii itakuwa inaonesha taarifa mbalimbali za Mahakama hii mfano ‘causelist’ ya kila wiki kwa kila Jaji na Msajili, taarifa za vikao maalum vya mashauri (Special Court Sessions), taarifa za kutokuwepo kwa Majaji na Wasajili ili kuokoa muda wa wadau ili wasifike mahakamani. Tovuti hii pia imeunganishwa na Tovuti ya Mahakama ya Tanzania ambapo imo mifumo mbalimbali ikiwemo Mfumo wa kuhifadhi hukumu za Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani, Sheria na Kanuni mbalimbali ‘TanzLII’,” amesema Mhe. Maghimbi.
Ameongeza kuwa, Tovuti hiyo imeunganishwa na tovuti za wadau muhimu ambao ni Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Chama cha Waajiri (ATE), Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Amesema uanzishwaji wa tovuti hiyo iliyotengenezwa na baadhi ya Watumishi/Wataalam wa ndani wa Divisheni hiyo unaenda sambamba na utekelezaji wa nguzo namba moja ya Mpango Mkakati wa Mahakama wenye lengo la kuboresha na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji haki na kuboresha miundombinu ya kitehama katika ngazi zote za Mahakama.
Kwa upande mwingine, Jaji huyo alimtaarifu Jaji Kiongozi kuhusu hatua kubwa waliyopiga kwenye umalizaji wa mashauri huku akibainisha kuwa, mpaka kufikia leo ni mashauri matatu (3) pekee ya mwaka 2021 yaliyobaki ambayo yote yako katika hatua ya hukumu na mpango uliopo ni mashauri hayo yawe yamemalizika ifikapo tarehe 06 Oktoba, 2022, na hivyo kubaki na mashauri ya mwaka 2022 tu.
Akitoa neno la utangulizi, Mwenyekiti wa Kamati maalum ya Utengenezaji wa Tovuti ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Biswalo Mganga amesema kuwa, tovuti hiyo imekidhi viwango vya kiusalama na mamlaka husika (eGA) wameridhia ianze kufanya kazi.
“Mahakama ya Kazi tuliona ni vizuri wananchi wafikiwe kwa urahisi zaidi pamoja na kuwakusanya wadau kwa pamoja kwahiyo njia mojawapo tuliyokubaliana kwa pamoja ni kuanzia tovuti ambayo imejumuisha pia tovuti za wadau wetu ili tuweze kuwasiliana kwa urahisi na kuwawezesha wananchi kupata taarifa mbalimbali kwa urahisi zaidi. Na niwahikishie kuwa Tovuti hii iko salama na tumezingatia vigezo vyote vya uanzishwaje wake,” amesema. Mhe. Mganga.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akibonyeza kitufe kwenye kompyuta mpakato kuashiria ufunguzi wa tovuti ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi leo tarehe 30 Septemba, 2022.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akizungumza kabla ya ufunguzi rasmi wa tovuti ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi akisisitiza jambo alipokuwa anaongea kwenye ufunguzi wa tovuti ya Mahakama hiyo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Biswalo Mganga, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati maalum iliyoundwa kwa ajili ya kuratibu utengenezaji wa tovuti hiyo akitoa maelezo mafupi jinsi inavyofanya kazi.
Sehemu ya Maafisa wa Mahakama ya Tanzania wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa Tovuti ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.Sehemu ya muonekano wa tovuti ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kushoto) akipokelewa na mwenyeji wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi (katikati) baada ya kuwasili kufungua rasmi tovuti ya Mahakama hiyo leo tarehe 30 Septemba, 2022 jijini Dar es Salaam. Wengine ni Jaji Augustine Rwizile (wa pili kulia) na Jaji Katarina Revokati Mteule (kulia).
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akisaini kitabu cha wageni ofisini kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Cassian Matembele akitoa utambulisho wa viongozi mbalimbali katika hafla fupi ya ufunguzi wa tovuti ya Mahakama hiyo.
Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi (juu na chini) wakifuatilia ufunguzi wa tovuti hiyo.
(Picha na Faustine Kapama, Mahakama)