Na Mwandishi wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt.Selemani Jafo leo Septemba 29, 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Sweden nchini Charlotta Ozaki Macias.
Pamoja na mambo mengine katika mazungumzo yao yalihusisha ushirikiano baina ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Nchi ya Sweden katika utekelezaji wa miradi ya utunzaji na hifadhi ya Mazingira.
Akizungumza katika kikao hicho jijini Dar es Salaam, Balozi Charlotta ameeleza miradi ya matumizi ya nishati mbadala inayotekelezwa kwa ufadhili wa Sweden kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa lengo la kupunguza uharibifu wa mazingira na uzalishaji wa hewa ukaa.
Amebainisha Sweden ilivyojizatiti kushirikiana na mataifa ya Afrika katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi hususan katika kushiriki mkutano wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika nchini Misri mwezi Novemba 2022.
katika kikao hicho, Balozi Charlotta ameambatana na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Scania Tanzania Johanna Lind ambaye amewasilisha mpango wa Kampuni hiyo wa kuingiza malori aina ya Scania yanayotumia gesi (Compressed Natural Gas -CNG) na BIOGAS badala ya Dizeli kwa lengo la kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na uchafuzi wa mazingira.
Mtendaji huyo ameeleza kuwa matumizi ya gesi ni rahisi na nafuu zaidi kuliko dizeli na kwamba changamoto iliyopo ni gharama zitokanazo na kodi na vituo vya kujazia gesi ambapo uwekezaji unahitajika.
Akihitimisha mazungumzo hayo, Waziri Jafo amemshukuru Balozi huyo kwa ushirikiano mzuri baina ya Tanzania na Sweden na kuahidi kuendeleza uhusiano huo mzuri hasa katika eneo la mazingira.
Aidha, amewapongeza Kampuni ya Scania kwa kuja na Mpango wa matumizi ya gesi katika magari yao na kuahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza Mpango huo na ikiwezekana uingizwe katika awamu ya tatu ya utekelezaji wa Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi.
Ujumbe mwingine ulioambatana na Balozi ni Joakim Ladeborn, Mkuu wa Kitengo cha Siasa na Biashara (Ubalozini) na Eliavera Timoth (Meneja wa Kitengo cha Biashara – Scania).