*************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Haiyo Yamati Mamasita amesema endapo atachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo, ndiyo ataamua ataachia nafasi gani kati ya hizo mbili.
Juzi Halmashauri kuu ya CCM Taifa ilirudisha majina matatu ya Haiyo Mamasita, Kiria Laizer na Anna Shinini ili wagombee nafasi ya Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Simanjiro.
Haiyo amesema hawezi kuahidi ataachia nafasi ipi hadi hapo uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya utakapokamilika na mshindi kutangazwa ukumbini.
“Huwezi kuchagua jina la mtoto ambaye bado hajazaliwa hivyo nitatangaza nitaachia nafasi ipi mara baada ya uchaguzi kufanyiwa hivyo kwa sasa siwezi kutamka chochote juu ya hilo,” amesema Haiyo.
Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Simanjiro amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kijiji Cha Landanai kwa muda wa miaka 10 na Diwani wa Kata ya Naberera kwa muda wa miaka mitano.
“Simanjiro ni yetu wote hakutatokea tatizo kwani hata hivyo majina yote matatu ya wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti yaliyorudishwa na Halmashauri kuu ya Taifa wana uwezo mkubwa,” amesema Haiyo.
Ameishukuru Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kuteua jina lake kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro kwani imempa heshima kubwa na kuonyesha imani kwake.
Amesema endapo atachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro atahakikisha anaongoza kwa upendo na kutobagua watu na kuondoa matabaka, makundi na makambi ya kisiasa ili Simanjiro iwe moja.
Katibu wa CCM wilaya ya Simanjiro, Amos Shimba amesema uchaguzi wa kugombea nafasi mbalimbali za wilaya hiyo unatarajiwa kufanyika Oktoba 2 mwaka huu kuanzia saa 4 asubuhi.
Shimba ametaja baadhi ya nafasi zitakazogombewa ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya, katibu mwenezi wa wilaya, wajumbe watatu wa mkutano mkuu wa Taifa na wajumbe wa mkoa na wilaya.