Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Morogoro Rufiji wameshiriki maonesho ya kilimo yanayoambatana na mbio maalumu kwa lengo la kuhamasisha na kutoa elimu kwa jamii ihusuyo umuhimu wa uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na kanuni zake.
Maonesho hayo yanayoadhimishwa katika viwanja vya Jamuhuri Mkoani Morogoro yenye kaulimbiu isemayo “Anzia Shambani” yamelenga pia kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya Sita ya Mhe Samia Suluhu Hassan ya kuinua kilimo na kuhamasisha vijana kujiajiri Ili waweze kujikwamua kiuchumi na kujenga uchumi wa maendeleo endelevu.
NEMC kwa upande wake kama mdau wa Mazingira katika maonesho haya yanayotarajiwa kufikia kilele siku ya Jumamosi tarehe 01/10 mwaka huu kwa mbio maalumu wamejikita katika kuelimisha si tu masuala ya Mazingira bali kilimo kinachozingatia tija na matumizi sahihi ya mbolea na viuatilifu.
Aidha NEMC pia wametoa elimu juu ya umuhimu wa uzingatiaji na ufanyaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira, umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji, umuhimu wa kutokuharibu ikolojia za mito na bahari Ili kuepukana na athari zinazoweza kujitokeza wakati wa uteketezaji wa shughuli za maendeleo hali itakayokuzuia kuyafikia malengo chanya katika kukuza uchumi endelevu.