*********************
Na Grace Semfuko, MAELEZO
Septemba 28, 2022
Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO Bw. Gerson Msigwa amewataka Viongozi wa Taasisi za Serikali Nchini, kutoa taarifa za mafanikio ya utendaji kazi wa taasisi hizo kwa Vyombo vya Habari, ili kuwaonesha Wananchi maendeleo yanayofanywa na Serikali yao.
Amesema yapo mambo mengi yanayofanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na hivyo ni muhimu kuyaweka wazi ili wananchi wayaone.
Ameyasema hayo leo Septemba 28, 2022 Jijini Dar es Salaam aliposhiriki mahojiano katika kipindi cha Baragumu kinachorushwa na Televisheni ya Channel Ten ikiwa ni Siku ya Kimataifa ya Upatikanaji wa Habari kwa Wote, na kubainisha kuwa wapo baadhi ya watendaji wanaokwepa kutoa taarifa za mafanikio ya taasisi zao kwa wananchi na kuwataka kuzitoa taarifa hizo.
“Wapo baadhi ya viongozi ni wakwepaji kuja kutoa taarifa kwenye vyombo vya Habari Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema, Mhe Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye ametoa maelekezo na Mimi Mwenyewe Msemaji Mkuu wa Serikali nimesema mara nyingi kwamba taasisi zote zinatakiwa kutoa taarifa kwa wananchi, zinatakiwa kuja kutoa ufafanuzi mbalimbali kwenye vyombo vya habari, wasije tu kwenye kampeni za kazi zao, wakati wote waje waseme wanafanya nini” amesema Bw. Msigwa.
Aidha amewataka Maafisa Habari wa Taasisi hizo pia kushirikiana na vyombo vya habari katika kutoa taarifa muhimu zinazohusu maendeleo ya taasisi zao.
“Lakini kwa kutambua kuna changamoto ya baadhi ya Viongozi kuwa na majukumu mengi, Serikali iliunda vitengo vya habari na nyie vyombo vya habari mkihitaji habari mnapaswa kuwasiliana nao ili muweze kupata taarifa na kuzitoa” amesema Bw. Msigwa.
Katika hatua nyingine Bw. Msigwa amewataka Wamiliki wa vyombo vya habari nchini, kuwalipa mishahara waandishi wao ili kuwajengea weledi katika kufanikisha kazi zao za kila siku.
“Nitoe wito kwa wamiliki wa vyombo vya habari tujitahidi sana kuwalipa watumishi tulionao ambao ni Waandishi wa Habari, wakifanya kazi zao walipwe kwa sababu tumepata hizo changamoto, na vyombo vya habari vinafanya kazi, waandishi wa habari hawana mishahara, wanategemea wakienda kufanya kazi kwenye taasisi fulani ndio walipwe posho, sasa hii sio sawa, ni vizuri vyombo vya habari vikawa na mipango madhubuti ya kuhakikisha waandishi wa habari wanapofanya kazi zao wanalipwa mishahara ili wafanye kazi kwa weledi” amesema Bw. Msigwa.