Ofisa Mawasiliano na Uhamasishaji wa ICAP akisikiliza swali kutoka kwa mmoja wa waandishi wa habari leo jijini Mwanza.Mshereheshaji maarufu nchini na Meya wa zamani wa Jiji la Dodoma, Peter Mavunde akichangia jambo katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Mwanza kuhusiana na uzinduzi wa Mradi wa Kitaifa wa Utafiti wa THIS 2022-2023 utakaofanyika kesho Rocy City Malls.Picha zote na Baltazar Mashaka
Bright Phiri wa ICAP (kushoto) akifafanua jambo kuhusiana na utafiti wa THIS 2022-2023 utakaozinduliwa kesho na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,George Simbachawene , kulia ni Ofisa Mawasiliano na Uhamasishaji wa ICAP, Mwanaidi Msangi.
NA BALTAZAR MASHAKA
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,George Simbachawene kesho Alhamisi atazindua utafiti wa pili kitaifa wa Viashiria na Matokeo ya VVU Tanzania (TANZANIA HIV IMPACT SURVEY-THIS 2022-2023) una.
Simbachawene atazindua utafiti huo jijini Mwanza kwa niaba ya Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa,ambapo utahudhuriwa na Naibu Waziri wa Afya,Dk.Godwin Mollel,Balozi wa Marekani nchini,Donald Wrigh,Mtakwimu Mkuu wa Serikali,TAMISEMI,wadau na sekta mbalimbali.
Mkurugenzi Mkazi wa ICAP,Haruka Maruyama alisema leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utafiti huo utakavyofanyika nchini katika mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar,ukilenga kuzifikia kaya takribani 20,000 sawa na watu 40,000.
Alisema utafiti huo wa pili utatathmini kushamiri kwa maambukizi mapya ya VVU na matokeo ya huduma za VVU katika jamii na kuangalia malengo ya Umoja wa Mataifa ya kudhibiti UKIMWI (UNAIDS) 95-95-95.
Mayaruma alisema THIS 2022-2023 utatumia dodoso la kukusanya taarifa za upimaji wa VVU,Homa ya Ini B na Homa ya Ini C kwa hiari,ikihusisha kaya takribani 20,000 sawa na watu 40,000 wenye umri wa miaka 15 na kuendelea kutoka aya zilizochaguliwa na kuridhia kushiriki.
Pia fursa ya upimaji wa VVU itatolewa kwa hiari na usiri katika kaya,ni muhimu wanakaya kupima na kufahamu hali zao za maambukizi ya VVU ikiwemo Homa ya Ini B na C, watakaobaini wataunganishwa na huduma za tiba matunzo ili kuisaidia serikali na wadau wengine kuboresha huduma za afya,sera na mipango ya kudhibiti maambukizi ya VVU nchini.
“THIS 2023-2023 ni utafiti uliofanywa na Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali (ICAP) lililopo Chuo Kikuu cha Columbia Marekani,kwa usaidizi wa kitaalamu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa na ufadhili wa Serikali ya Marekani chini ya Mfuko wa Dharura wa Kupambana na UKIMWI,ukilenga kutathmini matokeo ya afua mbalimbali za kinga,tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU,” alisema Mayaruma na kuongeza;
“Utafiti huo utatoa mwongozo kwa serikali na wadau wengine kutekeleza malengo ya UNAIDS 95-95-95 ya kudhibiti janga la UKIMWI kufikia 95 asilimia ya watu wote wanaioshi na VVU kufahamu hali zao, 95 ya waliogundulika watapatiwa huduma za matibabu na asilimia 95 wanaoishi na VVU wajue kiwango cha VVU mwilini.”
Alisema taarifa za utafiti huo ni muhimu,zitasaidia Tanzania kufikia malengo ya 95-95-95 na kuweza kudhibiti VVU ifikapo 2030,pia utafiti utatumika kupima maambukizi ya homa ya ini B na homa ya ini C kwa hiari.
Mayaruma alisema THIS 2022-2023 ni mwendelezo wa ule awali wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi uliofanyika katika ngazi ya kaya Oktoba 2016 hadi Agosti 2017, hivyo utawapa viongozi wa serikali,wafanyakazi wa afya,asasi za kiraia na watafiti,mwongozo wa kipekee wa kufanya maamuzi juu ya sera ya VVU,programu,ufadhili na kuwezesha familia kuwa na afya bora na taifa lenye ustawi.
Aidha kitaifa utafiti huo utahusisha kaya za maeneo mbalimbali ili kufahamu idadi ya maambukizi mpya ya VVU,ushamiri wa VVU/UKIMWI na waliopo katika matibabu ni miongoni mwa washiriki kuanzia umri wa miaka 15 na kuendelea.
Mkurugenzi huyo Mkazi wa ICAP alieleza kuwa ushauri nasaha utatolewa,watafiti watachukua sampuli ya damu kutoka mkononi kwa ajili ya kupima,majibu yatatolewa siku hiyo hiyo na watakaobainika kuwa maambukizi ya VVU watapewa rufaa katika vituo vya afya walivyochagua kwa usimamizi zaidi na usiri utazingatiwa.
Aliongeza THIS 2022-2023 itatoa mwongozo ngazi ya kitaifa katika kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa taarifa,kuongeza miundombinu ya maabara na uwezo wa rasilimali watu,taarifa za uelewa wa kina kuhusu mwitiko wa kitaifa katika kudhibiti VVU,mgawanyiko wa tabia hatarishi za VVU na utumiaji wa huduma za tiba na matunzo zitatolewa.
Kwa mujibu wa takwimu kiwango cha maambukizi ya VVU kitaifa ni kiwango cha 4.2 Tanzania Bara ambapo Mkoa wa Njombe unaongoza kwa kuwa na kiwango cha 11.4,Iringa 11.3,Mbeya 9.3,Mwanza 7.2,Kagera inafuatia ikiwa na kiwango cha 6.5 ambako ndiko mgonjwa wa kwanza alipatikana hapa nchini 1981.
Takwimu za matumizi ya dawa za kufubaza (ARV’s) Mkoa wa Lindi unaongoza kwa kiwango cha zaidi ya 100,Kilimanjaro 66.8,Kagera 66.0,Songwe 64.6,Pwani 63.5,Mara 63.4,Dodoma Njombe 60.5 huku mikoa inayobaki ikiwa chini ya kiwango cha 60 cha matumizi ya dawa hizo.
Kwa upande Zanzibar Mkoa wa Kaskazini Unguja, unaongoza kwa matumizi ya dawa za ARV’S ukiwa na kiwango cha 44.5 ikielezwa sababu ni mwingiliano wa watu kibiashara na utalii ambapo Mjini Magharibi una asilimia 21.0.