Balozi wa Tanzania nchini
Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo amesema takribani wawakilishi wa Kampuni
1,000 za nchini Italia wamethibitisha kushiriki kwenye Kongamano la Pili la Biashara
na Uwekezaji linalotarajiwa kufunguliwa rasmi jijini Zanzibar tarehe 28
Septemba 2022.
Akizungumza leo tarehe 27
Septemba 2022 jijini Zanzibar wakati wa mkutano wa maandalizi uliokuwakutanisha
Wawekezaji na Wafanyabiashara kutoka Italia na Maafisa wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar kutoka Sekta zinazosimamia masuala ya Biashara na Uwekezaji, Mhe.
Kombo amesema mwitikio huo mkubwa wa washiriki wa kongamano kutoka Italia unatokana
na jitihada zinazofanywa na ubalozi katika kutangaza fursa za biashara,
uwekezaji na utalii nchini humo.
“Ubalozi wa Tanzania nchini
Italia umeendelea kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa kutangaza fursa
mbalimbali za uwekezaji, utalii na biashara zilizopo nchini. Ni kutokana na
jitihada hizo Kampuni nyingi zimehamasika na kuonesha nia ya kuja kujionea
fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zitakazowasilishwa wakati wa
Kongamano hili. Nimefarijika sana kuona mwitikio huu wa washiriki kutoka Italia
ambao umezidi ule wa kongamano la kwanza” amesema Balozi Kombo.
Kadhalika ameongeza kusema
kuwa tayari zipo Kampuni kadhaa za Italia zimewekeza nchini ikiwemo ile ya Toscana
Macchine Calzature (TMC) iliyopo mkoani Kilimanjaro inayojishughulisha na
uuzaji wa mashine za kisasa na vipuri vyake vya utengenezaji wa viatu na bidhaa
na ngozi. Amesema Kampuni hiyo ambayo huzalisha viatu zaidi ya jozi 4,000 kwa
siku, imeonesha utayari wa kutoa wataalam saba (7) watakao toa mafunzo ya
utengenezaji bidhaa za ngozi katika Chuo cha Mafunzo Zanzibar.
Vilevile, Balozi Kombo ameeleza
kuwa, kutokana na jitihada zinazofanywa na ubalozi kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali wa utalii hapa nchini safari za ndege za watalii kutoka Italia
zimeongezeka kutoka safari tatu hadi nane kwa wiki.
Balozi Kombo alitumia fursa
hiyo kutoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa za soko la bidhaa kama
Parachichi ambazo tayari zimeanza kuuzwa nchini Italia.
Kwa upande wake, Balozi wa Italia
hapa nchini, Mhe. Marco Lombardi amepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali
ya Tanzania katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji na
kwamba nchi yake itaendelea kushirikiana Tanzania katika kukuza biashara na
uwekezaji baina ya nchi hizi mbili.
Kongamano hilo ambalo litafunguliwa
rasmi tarehe 28 Septemba 2022, linalenga
pamoja na mambo mengine kujadili kwa kina namna ya kukuza na kuimarisha
ushirikiano kati ya nchi hizi mbili kupitia sekta ya biashara na uwekezaji. Pia
kutoa nafasi kwa Tanzania kuainisha fursa za biashara na uwekezaji zilizopo
nchini zinazoweza kuchangamkiwa na washiriki kutoka Italia.
Kongamano hilo ambalo ni mwendelezo
wa Kongamano la Kwanza la aina hii lililofanyika jijini Rome, Italia mwezi
Desemba 2021, linatarajiwa kuhitimishwa jijini Dar es Salaam tarehe 30 Septemba
2022.
Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akiwa na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi wakiongoza kikao cha maandalizi ya Kongamano la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia kilichowakutanisha Maafisa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutoka Sekta zinazosimamia masuala ya Biashara na Uwekezaji na Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka Italia kwa ajili ya kubadilishana mawazo kuhusu mahitaji ya wawekezaji hao na fursa zilizopo nchini. Kikao hicho kimefanyika Zanzibar tarehe 27 Septemba 2022. Kongamano hilo litafunguliwa rasmi mjini hapa tarehe 28 Septemba 2022.
Mhe. Balozi Lombardi akizungumza wakati wa kikao cha maandalizi ya Kongamano la Pili la Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia |
Washiriki kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Wawekezaji na Wafanyabiashara kutoka Italia wakati wa kikao baina yao |
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Bw. Sharif Ali Sharif akifuatilia kikao |
Bw, Daniele Ferradini, Meneja Mauzo wa Kampuni ya TMC ya Italia inayojishughulisha na uuzaji mashine za kutengenezea viatu na bidhaa za ngozi iliyopo Kilimanjaro akichangia jambo wakati wa kikao
Kikao kikiendelea |
Kikao kikiendelea |
Sehemu ya Maafisa Waandamizi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakifuatilia kikao |
Afisa Mambo ya Nje kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Salma Baraka akinukuu mazungumzo wakati wa kikao |
Kikao kikiendelea |
Mwekezaji kutoka Italia akizungumza wakati wa kikao |
Mwekezaji kutoka Italia akichangia jambo wakati wa kikao |
Picha ya pamoja |