Kiwanda cha Flamingo Foods Kama kinavyoonekana wakati mwenge wa Uhuru 2022 ulipofika kukikagua.
………………………….
Wakulima wa mpunga katika Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi wameanza kunufaika na uwepo wa kiwanda cha kuchakata mpunga cha Flamingo Foods kilichopo katika Kijiji cha Ikaka kata ya Mnyagala katika tarafa ya Mwese.
Manufaa wanayopata wakulima hao ni pamoja na kuondokana na adha kusafirisha mpunga kupeleka katika Manispaa ya Mpanda kwa ajili ya kukobobolewa na badala yake shughuli zote zinafanyika kiwandani hapo.
Wakulima hao wamesema kuwa sasa Wana uhakika wa soko kwani wanauza kwa wakati.
Aidha kiwanda hicho pia kinaongeza thamani ya zao la mpunga kwa kuchakata na kuwekwa madaraja hali inayoongeza ubora na uhakika wa soko nje ya mkoa wa Katavi na nje ya nchi.
Kiwanda hicho ambacho kimewekeza zaidi ya shilingi milioni mia saba kina uwezo wa kuchakata tani sitini za mpunga kwa siku.
Aidha kiwanda hicho kinachoendeshwa na Vijana kimeajiri wafanyakazi watatu wa kudumu na wafanyakazi wa muda ishirini kiashiria kinachoonyesha kinaunga mkono serikali katika kuongeza ajira kwa Vijana.
Flamingo Foods Company ltd iliyoanzishwa Januari 5, mwaka huu kwa dhana ya kutimiza ndoto ya kuwa na Tanzania ya Viwanda ina vyumba viwili vya mashine, ghala la mpunga na ghala la kuhifadhia mchele ambapo kiwanda kipo katika eneo la ukubwa ekari tano walilonunua kwa shilingi milioni kumi na mbili.