Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa leo tarehe 27 Septemba, 2022 amefungua rasmi mabweni mawili yaliyojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Elimu wa Taifa unaosimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa ajili ya wanafunzi wa kike wa shule ya Sekondari ya Kainam ya Mbulu mkoani Manyara.
Akifungua mabweni hayo, Mhe. Bashungwa ameipongeza TEA kwa kazi nzuri wanayofanya katika kuboresha miundombinu ya elimu nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mabweni hayo.
Awali akizungumza kuhusu mradi huo, Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kainam, Bw. Atnasi Massay amesema mradi huo umesaidia wanafunzi kufanya vizuri kwani umewaepusha na vishawishi kwa kuishi katika mazingira ya utulivu.
“Kupitia mradi huu wa mabweni watoto wetu wamepata fursa ya kusoma na kupata utulivu na taaluma ya shule yetu imekuwa kwa maana sasa ni ya kwanza katika Halmshauri ya Mji wa Mbulu kitaaluma kwa matokeo ya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne na cha pili mwaka 2020 na 2021” anasema mwalimu huyo ambaye ameipongeza Serikali kwa kufadhili miradi hiyo.
Kwa upande wake Meneja Miradi wa TEA, Masozi Nyirenda amesema TEA kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa imetumia kiasi cha Sh. Bilioni 1.39 katika miradi mbali mbali katika mkoa wa Manyara katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015/2016 – 2019/2020.