Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani, alhaj Abubakari Kunenge amezindua mbio za Wakala wa Barabara ( TANROADS )Coast City Marathon ambayo inalenga kuhamasisha masuala ya Uwekezaji na viwanda Mkoani humo.
Kilele cha mbio hizo kinatarajiwa kufanyika Novemba 12 mwaka huu.
Akizungumza na wadau mbalimbali, wadhamini wa mbio hizo Wakala wa hifadhi za Misitu (TFS), NMB, ,NSSF na wadhamini wakuu TANROADS , Kunenge alieleza michezo ni suala muhimu katika kujenga afya na ameahidi nae kushiriki kukimbia kilometa 21.
Aidha alieleza ,mkoa huo ni ukanda wa viwanda hivyo kupitia mbio hizo utaongeza wigo wa kujitangaza na kufungua milango kwenye sekta ya uwekezaji.
“Mkoa wetu kwasasa una viwanda 1,460 kati ya hivyo vikubwa 90 ambapo vya kati ni 138 ,tunahakikisha kuboresha miundombinu,kuweka Mazingira Bora ya uwekezaji kwa ajili ya kuwavutia kwa kasi”
“Rais wetu Samia Suluhu Hassan anasisitiza kuinua sekta ya uwekezaji na viwanda na sisi Kama mkoa tunatekeleza kwa vitendo kwani Pwani HATUNA DOGO “alisisitiza Kunenge.
Wakati huo huo, Kunenge anawakaribisha wawekezaji, wafanyabiashara na wananchi kujitokeza katika maonyesho ya viwanda na biashara yatakayofanyika octoba 5-octoba 10 mwaka huu.
Nae Mwenyekiti wa Coast City Marathon, Frank Muhamba alieleza kilele kitakuwa Novemba 12 , na mazoezi yatakuwa yakifanyika kila jumamosi kuanzia Sasa hadi siku ya kilele.
“Umbali wa mbio utahusisha kilometa 21, kilometa 10, kilometa 5 hadi 2, “alifafanua Muhamba.
Mwakilishi wa Kanda ya Mashariki (TFS) ,Shaban Kiula aliwakaribisha wawekezaji kwenye maeneo ya uhifadhi Kanda ya Mashariki ili kuinua sekta ya utalii.