Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoani Tabora Mhandisi Raphael Stanslaus Mlimaji akiongea na Mwandishi wa Makala haya Ofisi kwake juzi.
Ujenzi wa daraja la Ibumba lenye urefu wa mita 60 katika makutano ya mto Wala na Kasisi katika barabara ya Tutuo-Usoke linalounganisha wilaya 3 za Sikonge, Uyui na Urambo ambayo liko katika hatua za mwisho za ujenzi linalojegwa kwa gharama ya sh bil 1.9
Mwonekano wa barabara ya Tabora-Sikonge-Mpanda kwenye mzunguko daraja la Mto Koga ambalo lilikuwa kikwazo kikubwa cha uchumi wa wakazi wa Mikoa hiyo 2 ya Tabora na Katavi barabara hiyo imekamilika kwa asilimia 100 na tayari imeanza kuwanufaisha wakazi wa Mikoa hiyo miwili baada ya kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan hivi karibuni
……………………..
Na Lucas Raphael,Tabora
Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa Mikoa michache yenye fursa lukuki za kiuchumi ambazo zilikuwa hazitumiki ipasavyo kutokana na changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara.
Ujenzi wa barabara za lami zinazounganisha Mkoa huo na Mikoa mingine ikiwemo wilaya zote 7 kuunganishwa kwa mtandao wa barabara za lami kumerahisisha usafiri na usafirishaji bidhaa hivyo kutoa fursa kwa wafanyabiashara, wakulima na wafugaji kunufaika.
Mkoa wa Tabora ambao miaka 5 hadi 10 iliyopita Ulikuwa na miundombinu mbovu ya barabara kuu zinazoingia na kutoka katika Mkoa huo.
Katika kutekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) wamefanikiwa kuzifanyia matengenezo barabara zote kuu kwa weledi mkubwa hivyo kufungua ukurasa mpya wa uchumi wa Mkoa huo.
Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tabora anaeleza
Mhandisi Raphael Mlimaji anaeleza kuwa ujenzi wa barabara za lami
katika mkoa huo umeboresha mazingira ya Mkoa na wilaya zake na
kufungua ukurasa mpya wa uwekezaji katika sekta mbalimbali.
Anafafanua uwekezaji ambao umeanza kushika kasi kuwa ni ujenzi wa
hoteli za kisasa na za kawaida, ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya
nyuki na bidhaa nyinginezo ikiwemo viwanda vya maji safi, maziwa,
juisi, mashine za kusaga na kukoboa na usindikaji bidhaa.
Anabainisha kuwa ujenzi wa barabara za lami katika Mkoa huo ulianza
kushika kasi katika mwaka wa fedha 2009/2010 ambapo miradi mingi
ilianza kutekelezwa na serikali na kukamilika kati ya mwaka 2014 – 2017
ambapo jumla ya km 383 zilijengwa kwa gharama ya takribani sh bil.445.3.
Hali ya barabara kwa sasa
Anabainisha kuwa barabara zote zinazounganisha Mkoa huo na Mikoa
mingine sasa zimetengenezwa kwa kiwango cha lami hivyo ukitoka Dar,
Morogoro, Dodoma, Arusha, Singida, Mwanza, Shinyanga na Katavi
unapita kwenye lami hadi Tabora.
Anaongeza kuwa barabara ya Kigoma -Tabora wakandarasi 2 wanaendelea
na kazi kwa kasi kubwa na baadhi ya maeneo tayari lami imeshawekwa,
maeneo yote yaliyokuwa hatarishi kwa kukosa madaraja sasa
yamejengwa na kupitika wakati wote na Mkoa sasa umefunguka kiuchumi.
Mhandisi Mlimaji anaeleza kuwa Mkoa sasa una mtandao wa
barabara wenye jumla ya km 2,187 zinazohudumiwa na TANROADS.
Anafafanua kuwa kati ya barabara hizo km 967 ni barabara kuu na km
1,220 ni Barabara za Mkoa (zikiwemo km 63 za wilaya), na kuongeza kuwa
kwa barabara za Mkoa asilimia 48 ziko vizuri, asilimia 47 wastani na
asilimia 5 zipo katika hali mbaya.
Barabara za lami
Mhandisi Mlimaji anaeleza kuwa Mkoa huo sasa una barabara za lami zenye urefu wa km 849.6 ambapo km 772 ni barabara kuu, km 53 za Mkoa na km 3 za wilaya hivyo kuunganisha Mkoa huo na Mikoa jirani.
Anaongeza kuwa katika mtandao huo barabara kuu ambazo
hazina lami ni km 195, za Mkoa km 1,105 na za Wilaya km 60, na jumla
ya madaraja 596 yamejengwa kwenye mtandao huo.
Aidha anaeleza kuwa katika mtandao wa barabara za lami asilimia 51
ziko katika hali nzuri, asilimia 48.4 ni za wastani na asilimia 0.4 haziko
vizuri, wakati zile za changarawe asilimia 85 zipo vizuri, asilimia 15 ni za
wastani na hakuna iliyo katika hali mbaya.
Miradi iliyotekelezwa
Anaeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya sh.bil 23.6 ziliidhinishwa kwa matengenezo ya barabara na ukarabati ambapo kati ya fedha hizo sh bil 21.09 ni za Mfuko wa Barabara (RFB) na sh bil 2.5 Mfuko wa Maendeleo.
Aidha jumla ya mikataba 56 yenye thamani ya sh bil 21.09 ilisainiwa kwa kazi mbali mbali za matengenezo ya barabara na madaraja ambapo utekelezaji barabara kuu umefikia asilimia 88.2 na za mkoa asilimia 88.3 hadi kufikia mwezi huu wa Septemba 2022.
Aidha katika mwaka huo wa fedha bajeti iliyopitishwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ilikuwa sh bil. 2.5 ambapo jumla ya mikataba 8 ya matengenezo ilitiwa saini na utekelezaji sasa umefikia asilimia 91 ya lengo.
Anataja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa daraja la Ibumba lenye urefu wa mita 60 kwa gharama ya sh bil 1.9 lililoko wilayani Sikonge (kazi inaendelea), barabara ya Kazilambwa – Chagu km 36, (sasa imefikia asilimia 60), barabara ya Malagarasi-Ilunde-Uvinza (imefikia asilimia 60), barabara ya Tabora-Koga-Mpanda km 356 (bil 32) na upanuzi wa uwanja wa ndege Tabora km 379 .
Mradi wa Uwanja wa ndege Tabora Anaeleza kuwa mradi huu ni fursa muhimu sana ya kukuza utalii na uchumi wa Mkoa kwani utahamasisha wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi kuja Tabora kwa kuwa usafiri ni mzuri.
Anafafanua kuwa jumla ya sh bil 3.6 zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha mradi huo na kati ya fedha hizo sh mil 602.20 ni fedha za ndani na sh bil 3.03 ni fedha za nje kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), mradi huu upo kwenye hatua za marekebisho ya gharama za mradi ili kuanza ianze.
Miradi itakayotekelezwa mwaka huu 2022/23
Mhandisi Mlimaji anasema Serikali imeidhinishwa jumla ya sh bil 25.7 kwa ajili ya kazi ya matengenezo na ukarabati wa barabara Mkoani hapa, fedha hizi zinajumuisha sh bil 22. 8 za Mfuko wa Barabara na sh bil 2.9 za Mfuko wa Maendeleo.
Aidha jumla ya mikataba 54 yenye thamani ya sh bil 22.8 na mikataba 14 yenye thamani ya sh bilioni 9.3 imesainiwa na mikataba 39 yenye thamani ya sh bil 13.6 iko katika hatua za uthamini, wakati mkataba 1 upo katika hatua za kutangazwa.
Mtendaji Mkuu TANROADS atoa aahadi nzito Mtendaji Mkuu TANROADS Mhandisi Rogatus Matwivila anaeleza kuwa wataendelea kutekeleza miradi yote iliyobainishwa katika mpango wa taifa wa maendeleo wa kipindi cha miaka mitano mitano ikiwemo ahadi za viongozi, ilani ya CCM na Vision 2025.
Aidha anabainisha kuwa watahakikisha miradi yote ya ujenzi wa miundombinu ya barabara za Kitaifa, Mkoa na za Wilaya ikiwemo madaraja, makaravati na mengineyo vinatekelezwa kwa ubora na viwango vinavyotakiwa ili kuchochea kazi ya maendeleo.
Anawataka wananchi kujivunia miradi hiyo kwa kuwa serikali imewajengea ili kuwaondolea kero, kuchochea kasi ya maendeleo yao na kutengeneza fursa za uwekezaji.
Anawahakikishia kuwa Wakala wa Barabara Tanzania ataendelea kutekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi kwa kasi kubwa ili kuharakisha maendeleo ya Mikoa na Wilaya zote nchini ikiwemo jamii kunufaika na fursa za uwepo wa barabara nzuri.
Miradi mipya ya barabara Anabainisha ujio wa miradi mipya ya kimkakati ambayo itaendelea kuufungua zaidi Mkoa huo kiuchumi kuwa ni Mradi wa Barabara wa Mpanda-Ugala Kaliua-Ulyankulu- Kahama ambao umetengewa jumla ya sh bil 5 kwa ajili ya kukamilisha usanifu ili kuanza ujenzi wake kwa kiwango cha lami.
Barabara nyingine ni Ipole-Rungwa (km172) ambayo imetengewa sh bil 5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, ujenzi unatarajia kuanza muda wowote.
Mradi mwingine ni wa Tabora-Mambali-Bukene-Itobo na Nzega-Kagongwa(km 180) ambao umetengewa jumla ya sh bil 1 kwa ajili maandalizi ya kuanza ujenzi w barabara kwa kiwango cha lami, ujenzi unatarajia kuanza muda wowote.
Mkuu wa Mkoa ampongeza Rais Samia Suluhu Hassan
Balozi Dkt Batilda Burian anampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya 6 Mhesh Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha za kutosha kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta zote.
Aidha anampongeza Kaimu Meneja Mhandisi Mlimaji kwa kazi nzuri ya usimamizi miradi ya barabara katika Mkoa huo na kuongeza kuwa kujengwa kwa barabara za lami katika Mkoa huo kumefungua fursa lukuki za kiuchumi na sasa Mkoa unang’aa, umekuwa TORONTO YA UNYAMWEZINI, UTAMU MWANZO MWISHO.
Wananchi wanena Juma Hamad mkazi wa Igagala-Kaliua anaeleza kuwa sasa hawana shida ya usafiri tena kama ilivyokuwa zamani, hata wafanyabiashara na wakulima hawahangaiki tena kusafiri bidhaa au mazao yao.
Christina Hemedi mkazi wa Ipole-Sikonge anamshukuru sana Rais Samia Suluhu hassan kwa kuwajengea barabara za kisasa na kuwawekea taa za barabarani, na kubainisha kuwa sasa kijijini na mjini hakuna tofauti .
DC Kaliua aita wawekezaji Tabora Mkuu wa wilaya ya Kaliua Mkoani hapa Paul Matiko Chacha anaipongeza serikali kwa kazi kubwa iliyofanya ya kuufungua Mkoa huo na wilaya zake na kuufanya Mkoa huo kuwa miongoni mwa Mikoa inayovutia wawekezaji wengi.
Anatoa wito kwa Wawekezaji wa ndani ya nje ya nchi kuja kutembelea Mkoa huo na Wilaya zake zote na kujionea fursa mbalimbali ikiwemo mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta zote.