WAKATI Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ukisomwa bungeni kwa mara ya kwanza,Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoani Mwanza umekutana na viongozi wa serikali za wanafunzi,wataalamu wa TEHAMA,washauri na walezi wa wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kati kujadili changamoto na kuzitafutia ufumbuzi.
Pia NHIF imewataka wanafunzi wa vyuo hivyo mkoani Mwanza kujisajili na kujiunga na mfuko huo ili kuwapunguzia wazazi na walezi gharama za matibabu, wasisubiri hadi waugue.
Alisema licha ya changamoto mfuko huo umeongeza idadi ya wanafunzi waliojiunga na bima ya afya kutoka 15,000 mwaka 2020/21 hadi kufikia 21,565 mwaka 2021/22,hivyo mwaka huu wanatarajia kuwasajili wengi kutokana wingi wa vyuo na mwamko uliopo.
“Tumekutana na viongozi wa serikali za wanafunzi kujadili changamoto za mwaka jana ili kuzifanyia kazi,uzoefu tuliopata mwaka 2021/22 ili kufikia matarajioa tutahakikisha wanafunzi wapata huduma kwa kuzingatia maelekezo ya serikali,kuwa na bima ya afya shiari ni lazima ili kupata huduma za matibabu wanapougua masomoni,” alisema Mushahu.
Alisema wanafunzi wakijiunga na NHIF watawapunguzia wazazi na walezi mzigo wa gharama za matibabu ingawa baadhi hupewa fedha na kuzitumia kwa mambo mengine, pia kuepuka kuchelewesha malipo ya wanachama vyuo viache kutumia mifumo ya zamani isiyo rafiki na NHIF.
Meneja huyo wa NHIF alivitaka vyuo vifunge mifumo madhubuti itakayoviwezesha kupata huduma mbalimbali zikiwemo za usajili wa wanafunzi,maboresho ya huduma mbalimbali za mfuko, malipo ya wanachama na taarifa zao.
Alisema ucheleweshaji malipo unasababisha wanufaika kuchelewa kupata kadi zao na kuzua malalamiko kwa mfuko huo wanapokosa huduma,nia ya NHIF kila mmoja awe na bima ya afya na kuonya watoa huduma wasio waaminifu wanaoshirikiana na wanafunzi kuwahudumia wasio wanachama watawajibika kisheria kwa kusababisha hasara na matumizi makubwa kwa wasiostahili na hilo halitavulimiwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Uanachama ya NHIF,Paul Bulolo alisema agenda ya serikali ya kila mwanafunzi kuwa na bima ya afya wanaiunga mkono,wameweka mkakati kuwafikia wananchi wote wawe na uhakika wa matibabu na kuwataka wamiliki wa vyuo kuwasajili watumishi wao kwa kuchangia asilimia sita ya mishahara.
“Uendelevu wa mfuko unategemea uchangiaji wa kundi kubwa la wananchi,watumishi wa umma,madhehebu ya dini na wanafunzi ingawa fedha ya mwanafunzi ni ngumu,hadi Juni 2021/22 idadi ya waliojiunga na vyuo ni kubwa lakini waliojiunga na NHIF ni wachache, hivyo tuna kazi kubwa ya kusajili wanafunzi wengi vyuoni,”alisema.
Naye mwakilishi wa Rais wa TAHILISO,Kamishna wa Afya,Alphoncina Mahundi,alisema afya ina umuhimu wa pekee,mwanafunzi asiyechangia NHIF,akitumia kadi ya matibabu isiyo yake ni kosa kisheria,hivyo serikali zote za wanafunzi zihamasishe kujiunga na NHIF pamoja na kutumia ofisi za mfuko kutatua changamoto.
“Serikali za wanafunzi mbali na kushirikiana kuibua changamoto na kuzitafutia ufumbuzi, zishirikiane na washauri wa wanafunzi kuondoa hili la kadi za bima kukaa muda mrefu bila kuchukuliwa na walengwa,kila mmoja awajibike kuhakikisha wanafunzi wanajiunga na mfuko wa NHIF,”alisema.
Aidha mmoja wa wadau hao Liberatus Ndegeulaya, alishauri wanafunzi wanaotengenezewa kidhiditi namba lakini hawalipii kwa madai hawaugui, uwekwe mfumo wa kuwadhibiti kuhakikisha wanalipa,pia wenye bima binafsi za afya uandaliwe utaratibu waunganishwe na NHIF.