***************************
Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Kibaha Mjini ,Eline Mgonja amefanikiwa kutetea kiti chake baada ya kupata ushindi wa kishindo wa kura 165 kati ya kura 237 zilizopigwa kwenye uchaguzi wa Jumuiya hiyo.
Uchaguzi huo ambao ulifanyika Picha ya Ndege Wilayani Kibaha Mgonja aliwabwaga washindani wake wawili na kufanikiwa kurudi kwenye nafasi yake.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo msimamizi wa uchaguzi huo Nasir Mkalipa alisema, idadi ya wapiga kura ilikuwa 238 ambapo kura moja iliharibika na kufanya kura halali kuwa 237.
Mkalipa alisema ,Batuli Maelo alipata kura 72 huku Caroline Malekela akipata kura moja hivyo kumfanya Mgonja kuendelea kuwa mwenyekiti kwa kipindi cha pili cha miaka mitano mingine.
Akiwashukuru wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi mwenyekiti huyo alisema kuwa anawashukuru wanachama kuendelea kumwamini kwa mara nyingine umoja na mshikamano
Mgonja alieleza,lengo kuu ni kumkomboa mwanamke ili kumwondoa asiwe tegemezi kuwa na ushirikiano pamoja na kuachana na dhana kuwa mwanamke hawezi lakini wanaweza wanapaswa wajiamini na wasikate tamaa kuna kuchafuliwa na kusemwa vibaya wakati wa uchaguzi lakini wanapaswa kupambana ili kufikia malengo yao.
Ataendelea kutoa elimu ya ujasiriamali ambayo alikuwa akiitoa kama Mwalimu ambapo kwa sasa atatoa kwa kila kata kwa kuwafuata akinamama huko huko kwenye maeneo yao.
“Nawashukuru sana akinamama wenzangu kwa kunipa imani tena sitawaangusha ili kuweza kufikia malengo yetu ambayo tumejiwekea ya kujikwamua kiuchumi ili kufanya familia zetu ziwe na ustawi na kujiletea maendeleo,”alisema Mgonja.