Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) imefanya kikao chake cha 222 tarehe 23 Septemba 2022, ili kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo wa uchumi kwa kipindi cha mwezi Julai na Agosti 2022. Kamati imeridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha, uliotoa wigo wa kukuza shughuli za kiuchumi, licha ya kuwepo kwa changamoto zinazosababisha kupanda kwa mfumuko wa bei, kutokana na ongezeko la bei za bidhaa katika soko la dunia.
Kamati imeridhishwa pia na kasi ya ukuaji wa uchumi inayokwenda sambamba na matarajio, licha ya kuwepo na changamoto zitokanazo na ukuaji mdogo wa uchumi wa dunia, kupanda kwa bei za bidhaa katika soko la dunia, kuongezeka kwa mfumuko wa bei, hali ngumu ya kifedha duniani, pamoja na maambukizi mapya ya UVIKO-19 kwa baadhi ya nchi duniani. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2022, uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa asilimia 5.4, ikilinganishwa na makadirio ya asilimia 4.7 kwa mwaka 2022. Ukuaji huu umechangiwa zaidi na shughuli za kilimo, ujenzi, viwanda na uchimbaji wa madini. Kwa upande wa Zanzibar, uchumi umekua kwa asilimia 5.1, ikilinganishwa na makadirio ya asilimia 5.4 kwa mwaka 2022. Ukuaji huu unatokana na kuimarika kwa shughuli za utalii. Kutokana na mwenendo huu wa uchumi, kuna uwezekano mkubwa wa kufikia makadirio ya ukuaji wa uchumi kwa Tanzania Bara na Zanzibar kwa mwaka 2022.
Mfumuko wa bei nchini umeendelea kuongezeka, japo kwa kasi ndogo na kubaki katika wigo wa tarakimu moja. Mfumuko wa bei kwa upande wa Tanzania Bara umeongezeka na kufikia asilimia 4.6 mwezi Agosti 2022, kutoka asilimia 3.6 mwezi Machi 2022, kiwango ambacho bado kipo ndani ya lengo la wastani wa asilimia 5.4 kwa mwaka 2022/23. Mfumuko wa bei kwa upande wa Zanzibar, umeongezeka kufikia asilimia 5.4 kutoka asilimia 3.5, kiasi ambacho ni juu kidogo ya lengo la asilimia 5. Mwenendo huu umechangiwa na kupanda kwa bei za bidhaa katika soko la dunia, hususan vyakula na mafuta. Kwa kipindi kilichobakia cha mwaka 2022/23, mfumuko wa bei unatarajiwa kubakia ndani ya malengo kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia hivi karibuni, thamani ya Shilingi ya Tanzania kuendelea kuwa tulivu, na matarajio ya kupungua kwa kasi ya kupanda kwa bei za vyakula nchini.
Ujazi wa fedha umeendelea kuongezeka, ukichangiwa zaidi na kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi. Kwa kiasi kikubwa, ongezeko hili limetokana na utekelezaji wa sera wezeshi za fedha na bajeti, na kuimarika kwa mazingira ya kufanya biashara na shughuli za kiuchumi zilizokuwa zimeathiriwa na UVIKO-19. Ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) umeongezeka kwa asilimia 7.9 na asilimia 11.5 mwezi Julai na Agosti 2022, mtawalia, sanjari na lengo la asilimia 10.3 kwa mwaka 2022/23. Kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi imeongezeka na kufikia wastani wa asilimia 20, kwa mwezi Julai na Agosti, 2022 ikilinganishwa na makadirio ya asilimia 10.7 katika kipindi chote cha mwaka 2022/23.
Katika kipindi cha Julai na Agosti 2022, ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa Tanzania Bara, ulifikia asilimia 93.8 ya lengo, ambapo mapato ya kodi yalikuwa asilimia 95.9 ya lengo, huku matumizi yakiendelea kuwiana na rasilimali zilizopo. Kwa upande wa Zanzibar, mapato ya kodi yalikuwa asilimia 96.4 ya lengo, kufuatia kuanzishwa kwa matumizi ya mashine za kielektroniki (Electronic Fiscal Devices). Aidha, matumizi ya Serikali yameendelea kuwiana na rasilimali zilizopo.
Sekta ya nje imeendelea kukabiliwa na athari za ongezeko la bei za bidhaa katika soko la dunia na hali ngumu ya kifedha duniani. Hali hii imesababisha kuongezeka kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamishaji mali nchi za nje. Pamoja na changamoto hizo, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kubakia katika viwango vya kutosha na kufikia dola za Marekani milioni 5,092 mwishoni mwa mwezi Agosti 2022, kiasi kinachotosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takriban miezi 4.6. Kwa kuzingatia mazingira ya sasa na changamoto za kiuchumi duniani, Kamati ya Sera ya Fedha imesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni ili kudumisha utulivu wa thamani ya shilingi na kukidhi mahitaji ya nchi.
Kwa kuzingatia tathmini ya mwenendo wa uchumi wa Tanzania na changamoto za kuongezeka kwa mfumuko wa bei duniani, pamoja na kupanda kwa bei za bidhaa, Kamati ya Sera ya Fedha imeiridhia Benki Kuu ya Tanzania kuendelea kupunguza taratibu kasi ya kuongeza ukwasi kwenye uchumi katika kipindi cha mwezi Septemba na Oktoba 2022. Uamuzi huu unalenga kukabiliana na athari za kuendelea kuongezeka kwa mfumuko wa bei, sambamba na kulinda kasi ya ukuaji wa uchumi.
Gavana
Benki Kuu ya Tanzania