Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)Mjini Kibaha , Mkoani Pwani Ramadhani Kazembe amewaasa wanachama wa Jumuiya hiyo , kujituma na kuwa wazalendo wakati wote kwenye kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi ili kujiwekea akiba ya kuaminika kwenye nyanja za Uongozi.
Aidha amehimiza upendo, ushirikiano baina ya wanachama na viongozi pamoja na kuondoa makundi baada ya chaguzi zinazoendelea ndani ya Chama kumalizika.
Akishukuru wanachama wa UVCCM Kibaha Mjini, baada ya kutangazwa kushinda nafasi ya Mwenyekiti Mjini humo kwa kujinyakulia kura 177 ,Kazembe alieleza , kipindi cha nyuma alishika nafasi mbalimbali na kujitoa kwenye Jumuiya na Chama ,Jambo ambalo limejenga imani kwa wengine na kuonekana kiongozi bora na si bora kiongozi.
“Uvumilivu wangu ,kujitoa ,ubunifu na kuitumikia Jumuiya na Chama ndio imenifikisha hapa, nawashukuru sana vijana wenzangu, na nawashukuru hata ambao hawajanipa kura kwakuwa naamini huu ulikuwa ni uchaguzi”
“Niwaombe wenzangu ambao kura hazijatosha tuendelee kushirikiana, ili vijana wapige hatua ya kimaendeleo”
Hata hivyo,Kazembe alieleza ,mkakati wake ni kuwatumikia vijana na chama , kuongeza nguvu ya kutafuta vitega uchumi ili kuondokana na utegemezi sanjali na kuhakikisha makundi ya vijana yanawezeshwa kupitia mikopo ya halmashauri ili kujiongezea kipato.
Awali akitangaza matokeo ya uchaguzi wa UVCCM Kibaha Mjini yaliyofanyika ukumbi wa Triple J Pichandege Kibaha , msimamizi wa uchaguzi Katibu wa UWT Mkoa ,Fatuma Ndee alisema Kazembe ameshinda kwa kupata kura 177 kati ya kura 316 zilizopigwa ambapo kura nne ziliharibika.
Nafasi ya pili alishika Godlove Rwekaza ambae alikuwa akitetea kiti hicho na kuangukia kura 84 na watatu Nancy Matta aliyepata kura 55 .
Ndee alimtaja ,Mjumbe nafasi ya UVCCM wilaya kuwakilisha mkutano Mkuu Mkoa kuwa ni Valentine Mbawala , nafasi ya mjumbe Halmashauri Kuu ya CCM ni Jonas Ngwesa na mjumbe wa mkutano mkuu CCM wilaya Happiness Eustace.
Nafasi ya wajumbe wa Baraza la vijana wilaya Ally Gombati, Benjamin Mjata,Ashura Thomas,Mwasiti Nzota na Abuu Matumla.
Nae Katibu wa UVCCM Kibaha Mjini,Amina Makona alishukuru zoezi limeenda vizuri toka hatua ya uchukuaji fomu hadi kufanyika uchaguzi huru wa haki .
Aliomba waliochaguliwa kuendelea kujituma ,Kuwa wabunifu na utumishi uliotukuka .
Makona aliwaasa ambao hawafanikiwa kushinda wasikate tamaa ,kwani kumalizika kwa uchaguzi huu ni mwanzo wa chaguzi zijazo hivyo wasisite kuendelea kujitokeza kwenye chaguzi mbalimbali.