***********************
Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila imepokea msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya TZS 382,650,980 Mil kutoka serikali ya Korea Kusini kupitia Taasisi ya Korea Foundation for Health Care (KOFIH) vitakavyotumika kuboresha utoaji wa huduma katika wodi ya watoto wachanga mahututi.
Akikabidhi msaada huo kwa uongozi wa hospitali, Balozi wa Korea Kusini nchini Mhe. Kim Sun Pyo amesema serikali ya Korea Kusini itaendelea kuisaidia Tanzania katika eneo la mafunzo na kuboresha huduma za afya kupitia taasisi zake hususani KOFIH.
Mhe. Kim amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru kwa ushirikiano aliouonesha kwa taasisi za Korea Kusini katika kuboresha huduma za afya hospitalini hapa.
“Namtakia Prof. Museru maisha mema, tumekuwa na ushirikiano ambao kwa kiasi kikubwa umesaidia sana kuboresha huduma za afya katika hospitali hii. Tutaendelea kuhitaji ushauri na maoni yake kuendelea kuboresha huduma za afya nchini” amesema Mhe. Kim.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi akipokea msaada huo kwa niaba ya Wizara ya Afya, amesema utasaidia kuendelea kuboresha huduma za watoto wachanga mahututi kufuatia ukarabati wa wodi hiyo uliofanywa na KOFIH miezi michache iliyopita.
“ Vifaa hivi vilivyokabidhiwa leo vitasaidia kuongeza tija katika huduma za watoto wachanga mahututi kwa kuwa ni vingi na muhimu kwenye utoaji wa huduma, kwa niaba ya watumishi wenzangu tutahakikisha tunavitunza , kuvikarabati mara kwa mara na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa” amesema Dkt. Magandi
Msaada huo wa vifaa tiba ni pamoja na mashine ya kumsaidia mtoto kupumua, mashine ya kumsaidia mtoto kuondoa manjano (jaundice), mashine inayomsaidia mtoto kutunza joto la mwili kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (premature babies).
Mashine nyingine ni ya kufuatilia mapigo ya moyo ya mtoto akiwa tumboni mwa mama yake, mashine inayomsaidia mtoto ambaye hawezi kupumua mwenyewe na mashine ya kufuatilia ishara za mwili wa binadamu.
Kukabidhiwa kwa msaada huu kunafuatia kuzinduliwa kwa mtambo wa kuzalisha hewa tiba (Oxygen generating plant) wenye uwezo wa kuzalisha mitungi 200 ya ujazo wa 6.3 M³ kwa siku ambao umegharimu dola za Marekani 300,000, pamoja na mradi wa kuboresha huduma ya mama na mtoto uliohusisha uboreshaji wa wodi ya watoto wachanga mahututi (NICU) na kuanzisha Wodi ya Uangalizi Maalumu ya Wazazi (Maternal ICU) kwa gharama TZS 240,808,060 Mil.