NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, MOROGORO
MAAFISA Rasilimali watu na Utawala hapa nchini wamehimizwa kutumia TEHAMA wakati wa kutoa Taarifa kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) pindi Mfanyakazi anapoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi ili kuharakisha mchakato wa utoaji fidia.
Wito huo umetolewa mjini Morogoro Septemba 22, 2022 na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini wa Mfuko huo Dkt. Abdulsalaam Omar wakati akifungua Kikao Kazi cha Maafisa Rasilimali Watu na Utawala kutoka Taasisi na Mashirika ya Umma kuhusu Huduma zitolewazo na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na umuhimu wa kuzingatia Usalama na Afya Mahali pa Kazi.
“WCF imetimiza miaka saba (7) tangu kuanzishwa kwake, katika kipindi chote hicho tumefanya maboresho mengi ya utoaji wa huduma, hivyo kuongeza elimu kwa wadau juu ya huduma zetu ni jukumu la msingi.” Amesema
Alisema WCF inatambua dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya sita chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuwa na uchumi endelevu na kuboresha hali ya maisha kwa wananchi wake kwa kutoa huduma bora.
“Dhamira hii itawezekana pale ambapo tutakuwa na wafanyakazi wenye uhakika wa afya zao kazini na endapo itatokea bahati mbaya wakapata madhara wakiwa wanafanya kazi basi wawe na uhakika wa kupata Fidia stahiki na kwa wakati na kwa kutumia TEHAMA hili linawezekana.” Alisema Dkt. Mduma.
Pamoja na matumizi ya TEHAMA Maafisa hao wamehimizwa kuambatisha nyaraka muhimu wakati wa kuwasilisha Madai.
Vile vile amesema amesema matukio yanayotokea nje ya maeneo ya kazi mfano mfanyakazi anatoka nyumbani kwenda kazini au kazini kurejea nyumbani na au yuko katika safari ya kikazi na kwa bahati mbaya akapatwa na ajali lazima tukio hilo litolewe taarifa Polisi ambako atapatiwa PF3 kwa ajili ya matibabu na PF90 ambayo itaeleza jinsi ajali ilivyotokea na wahusika.
“Kwetu sisi nyaraka hizi ni muhimu sana, kwani ndizo zinathibitisha kuwepo kwa tukio na niwaombe ndugu washiriki, mfikishe ujumbe huu kwa wafanyakazi ili mchakato wa kulipa fidia uwe wa haraka.” Alibainisha Dkt. Mduma.
Akizungumzia ajali zinazotokea kwenye maeneo ya kazi Afisa Mafao Mwandamizi wa WCF, Bw. Silvanus Kuloshe amesema jicho la WCF ni Afisa Rasilimali Watu ambae atajaza fomu husika na kuziambatisha wakati wa kuwasilisha taarifa za Madai.
Kwa upande wao, washiriki wamesifu matumizi ya TEHAMA kwani yamekuwa yakirahisisha utoaji ya taarifa WCF pindi panapotokea matukio ya ajali au mfanyakazi akiugua.
“Mwanzo kulikuwa na changamoto wakati tukitumia mfumo wa kuwasilisha taarifa kwa dispatch…lakini mfumo huu wa WCF Portal umerahisisha uwasilishaji wa taarifa na hili ni jambo muhimu katika ulemwengu wa sasa.” Amesema Bw. Allan Gelege, mmoja wa washiriki
Naye Bi.Fatma Ramadhan, amesema amekuwa akitumia mifumo yote miwili, wa TEHAMA na ile ya kuwasilisha madai kwa dispatch,
Amesema Mfumo wa TEHAMA unatoa fursa ya kupata fomu zote zinazohitajika na hii imewarahisishia wanapohitaji kutoa taarifa pindi panapotokea tukio lolote na kumekuwepo na mawasiliano bora.
“Njia hii ni nzuri ukilinganisha na ile ya kutuma madaoii fisini kwa njia ya dispatch, ninawapongeza WCF kwa huduma hii kwani imekuwa rafiki katika mawasiliano baina yetu na wao.” Alifafanua Bi. Fatma ambaye yeye ni Afisa Rasilimali Watu Mwandamizi Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Dar es Salaam.