**********************
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
NAIBU Waziri wa Habari ,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew ameeleza , takwimu za Juni 2022 zinaonyesha Jumla ya miamala ya kifedha milioni 343 yenye thamani ya sh.trilioni 11.6 ilifanyika katika kipindi hicho.
Ameelezea, hilo ni ongezeko kutoka miamala milioni 330 yenye thamani ya sh.trilioni 10.7 mwezi Machi mwaka 2022 ambapo inaonyesha namna Tanzania inavyoelekea kwenye mfumo wa kifedha jumuisha .
Akifungua Semina ya kuelimisha na kuhamasisha watumiaji wa huduma za Mawasiliano ,Kibaha ,mkoani Pwani ,Kundo alieleza Serikali imeweka mikakati ya kuenea huduma za mawasiliano nchini kote.
Aidha alifafanua kuwa , hivi sasa simu za mkononi zimeenea kwa asilimia 92 ya Watanzania na internet kwa asilimia 48 ambapo wastani wa usajili wa laini nchi nzima ni laini milioni 1.9 kwa kila mkoa.
“Laini 1,630,142 zimesajiliwa mkoa wa Pwani ambao ni wa tano Kitaifa kwa uwiano wa laini na idadi ya watu, Mkoa unaoongoza ni Dar es salaam,ukifuatiwa na Arusha,Mbeya na Iringa.”
Kundo alieleza, Tanzania ina makampuni ya watoa huduma za simu za mkononi saba, ambao wamewezesha laini za simu 56,153,097 kusajiliwa hadi ilipofika mwezi Juni 2022 ukilinganisha na laini 41,833,834 mwezi juni 2018.
Alisema kutokana na tatizo kubwa ambalo linawakabili watumiaji wa huduma za mawasiliano ni kutokujua haki na wajibu wao pamoja na kutofahamu namna gani wataweza kutatua matatizo yao hususan huduma ambazo hazikidhi mahitaji ya mtumiaji.
Kundo alilisisitiza ,Baraza la watumiaji wa huduma za mawasiliano (TCRA CCC) liwe chombo cha kumuwezesha mtumiaji kujitambua katika kudai haki zake pamoja na kutimiza wajibu wake katika jamii.
“Kwa mantiki hii kazi za Baraza hili zilenge zaidi katika kumtetea mtumiaji na kumsaidia kuinua hali yake ya maisha ikiwa ni kushinikiza watoa huduma kusambaza huduma hizo kila pembe ya nchi”alielezea Kundo.
Alizitaka kamati za watumiaji wa huduma za mawasiliano zitekeleze majukumu Yao kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu ili kumwezesha mtumiaji wa huduma za mawasiliano,kujua haki na wajibu na kumwezesha mtumiaji kufanya maamuzi sahihi katika ununuzi wa huduma ama bidhaa hizo.
Awali Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la watumishi wa huduma za mawasiliano,Mary Msuya alieleza baraza hilo linaendelea kuchochea, uelewa wa watumiaji .
“Ndio maana hata leo tumeweza kuwakutanisha watumiaji,watoa huduma kubadilisha mawazo na Jeshi la polisi akiwa mdau muhimu kwenye uhalifu wa mitandao.”alisema Mary.
Sanjali na hayo,Mary alisema hadi sasa kuna kamati zilizoundwa 16 ikiwemo na mkoa wa Pwani kati ya kamati hizo ni pamoja na mbili za Tanzania Visiwani.
Mkuu wa wilaya ya Kibaha, Sara Msafiri alieleza mawasiliano ya mtandao yameongezeka Lakini wapo ambao wanatumia mitandao vibaya na kufanya vurugu.
Alisema , Ni wajibu wa Taasisi husika kudhibiti matukio ya uhalifu, kufanya udanganyifu na mizaha kwenye mitandao .