Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Mhandisi Benard Kavishe akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), wakati akitoa taarifa kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wahandisi Tanzania yatakayofanyika yanayotarajia kuanza kesho Septemba 22 na 23 2022, Jijini Dodoma.
……………………………………………………
Na Alex Sonna-DODOMA
MSAJILI wa Bodi ya Wahandisi (ERB) Mhandisi Bernadrd Kavishe ,amesema kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika siku ya maadhimisho ya 19 ya bodi ya usajili wa wahandisi nchini yanayotarajia kuanza kesho jijini Dodoma.
Hayo ameyasema leo Septemba 21,2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa maandalizi kwa ajili ya maadhimisho hayo yamekamilika.
Mhandisi Kavishe amesema kuwa wahandisi wapatao 35,000 watashiriki ambapo kwa wale watakoshindwa kuhudhuria watafuatilia kwa njia ya mtandao.
“Mkutano wetu pia utafanyika kwa njia ya mtandao (Zoom) ,maana sisi tuna wahandisi wapatao 3,500 na siyo rahisi wahandisi wote wakapata fursa ya kuhudhuria,kwa hiyo tumeona tufanye pia kwa njia ya mtandao ambapo itatoa fursa kwa wahandisi watakaoshindwa kuhuduria kutufuatilia kwa njia ya mtandao.”amesema
Hata hivyo amesema kuwa wahandisi 400 watakula kiapo cha utii na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia taaluma na hivyo kuuwezesha umma kujenga imani kwa wahandisi na kuthamini kazi za kihandisi.
Aidha Mhandisi Kavishe amesema kuwa wahandisi 200 kati ya 800 ambao wamechukuliwa hatua na Bodi ya Wahandisi nchini,kutokana na makosa mbalimbali,wamerudishiwa usajili
Maadhimisho ya siku ya wahandisi mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Ubunifu na Uendelezaji wa Ujuzi katika Kuimarisha Maendeleo Endelevu ya Uchumi wa Taifa: mtazamo wa kihandisi”.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Siku ya Wahandisi Benedict
Mukama amesema mpaka sasa tayari kila kitu kimekamilika,na kutakuwa na ugeni wa wahandisi kutoka nje ya nchi ili kuja kubadilishana mawazo na wahandisi wa hapa nchini katika masuala ya utendaji kazi zao za kila siku.