Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Dkt.Francis Michael ameutaka Uongozi wa Mamlaka ya Ufundi Stadi nchini (VETA) kujiandaa na mageuzi ya elimu ili kuhakikisha wahitimu wanaozalishwa na vyuo vilivyopo chini ya Mamlaka hiyo wanaajirika na kujiajiri.
Akizungumza na Uongozi pamoja na Watumishi wa VETA Makao Makuu jijini Dodoma, Dkt. Michael amesema dhamira ya Serikali ni kuwa na elimu itakayosaidia wahitimu kufikiria fursa zilizopo na kuzitumia ili kutengeneza maisha yao na kuchangia katika uchumi wa Taifa.
“Tunatakiwa tuzalishe wahitimu ambao wanafikiri na kuwa na uwezo wa kujitengenezea kipato kutokana na fursa zinazowazunguka, tumeamua kwenda kwenye elimu ujuzi (competence based) hivyo VETA lazima mjiandae ikiwemo kuanzisha kozi hadi za Kilimo.” amesema Dkt. Michael.
Katika ziara hiyo, Dkt. Michael pia alisikiliza na kutoa ufafanuzi juu ya changamoto mbalimbali kutoka kwa watumishi wa mamlaka hiyo.
Sanjari na hayo, Dkt. Michael ametembelea na kukagua kiwanda cha utengenezaji wa samani kinachomilikiwa na Mamlaka hiyo kilichopo jijini Dodoma.