MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein(kulia), akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mahusiano ya Nje ya Chama Cha Kikomunisti cha Vietnam Ndugu Truong Quang Hoai Nam(kushoto), ambaye ni kiongozi wa msafara wa Chama hicho kutoka Vietnam aliyefika Afisi Kuu ya CCM Zanzibar kwa ajili ya mazungumzo na Viongozi wa CCM.
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein(kulia), akimkabidhi zawadi maalum ya Kasha lenye zawadi mbali mbali ikiwemo Karafuu, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mahusiano ya Nje ya Chama Cha Kikomunisti cha Vietnam Ndugu Truong Quang Hoai Nam.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdalla Juma Mabodi(kulia), akikabidhi zawadi ya mfano wa jahazi Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mahusiano ya Nje ya Chama Cha Kikomunisti cha Vietnam Ndugu Truong Quang Hoai Nam.
****************
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema kitaendelea kuenzi mahusiano yake ya kisiasa baina ya Chama hicho na Chama Cha Kikomunistini cha Vietnam (CPV) ili wananchi wa pande zote mbili wanufaike na fursa za kiuchumi,kisiasa,kijamii na kidiplomasia.
Hayo yameelezwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein, wakati akizungumza na Ujumbe wa Viongozi wa Chama Cha Kikomunistini cha Vietnam (CPV) huko Afisi Kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui.
Dk.Shein, ameeleza kwamba mahusiano ya nchi hizo ni ya kihistoria na yameweza kuleta manufaa makubwa kwa Zanzibar.
Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alisema kwamba nchi hiyo imepata mafanikio makubwa katika nyanja zote zikiwemo za kiuchumi, kijamii na kisiasa na kueleza kuwa Zanzibar itaendelea kujifunza kutoka nchi hiyo.
Shein aliipongeza Vietnam kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo ambao umeweza kuleta mafanikio makubwa sambamba na mahusiano kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Kikomunisti cha Vietnam (CPV).
Makamu Mwenyekiti huyo Dk.Shein, amesema kuwa Zanzibar imepata maendeleo makubwa kutokana na usimamizi mzuri wa sera za Chama Cha Mapinduzi.
“ CCM ina muundo mzuri wa kiuongozi,kiutawala,kiutendaji na kimkakati unaofanya kazi katika pande zote za nchi mbili za Zanzibar na Tanzania Bara.
Hivyo vipaumbele vya sera zetu vinajielekeza katika kukuza uchumi wa nchi ili wananchi wawe na kipato cha kutosha na kujikimu kimaisha”, alisema Dk.Shein.
Pamoja na hayo alieleza kwamba Chama Mapinduzi kimekuwa na muundo wa kiungozi kuanzia ngazi za Mashina hadi Taifa hatua inayotoa fursa sawa kwa kila mwanachama kugombea nafasi anayotaka.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mahusiano ya Nje ya Chama Cha Kikomunisti cha Vietnam Ndugu Truong Quang Hoai Nam,amesema lengo la ziara hiyo ni kujifunza na kupata uzoefu kutoka CCM ili kupata siri mafanikio katika masuala ya kisiasa,kiuchumi,kijamii,kiuongozi na kidiplomasia.
Ndugu Quang, alisema pamoja na hatua za kimaendeleo zilizofikiwa katika nyanja mbalimbali nchini Vietnam bado wanahitaji kuendelea kujifunza zaidi masuala utalii,uwekezaji,siasa na itikadi kutoka nchi rafiki ikiwemo Zanzibar.
Makamu Mwenyekiti huyo alikipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kuongoza kwa mafanikio makubwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo kwa sasa imeendelea kuheshimika kimataifa.
Pamoja na hayo alieleza kwamba ziara hiyo itakuwa chachu ya kuendeleza mahusiano ya kubadilishana mbinu,uzoefu,mafunzo na mikakati ya kuyajengea uwezo makundi ya vijana na wanawake waweze kujiajiri wenyewe.
“Tumeona fursa nyingi Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zinazoweza kuwakwamua kiuchumi wananchi na wakaweza kujitegemea kupitia sekta za kilimo,uvuvi,ufugaji na utalii.”, alisema Ndugu Quang.
Akizungumza na ujumbe huo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi, alisema ushindi wa Chama Cha Mapinduzi unatokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2022.
Dk.Mabodi, ameeleza kuwa kupitia mazungumzo hayo CCM imeshauri Vietnam kuwajengea uwezo na kuwapatia mafunzo ya Kilimo cha mpunga cha umwagiliaji,uvuvi,ujasiriamali na uendeshaji wa viwanda vidogo vidogo.
Alisema kuwa ujumbe huo wameeleza nia yao kuwa na mpango wa kuongeza watalii nchini pamoja na kuimarisha mahusiano ya kisiasa,kiuchumi na kidiplomasia.
Alifafanua kwamba CCM imewaeleza viongozi hao namna Serikali inavyotekeleza sera za Uchumi wa Blue pamoja na Royal Tour ili kuhakikisha mataifa ya nje yanawekeza Zanzibar na wananchi wanapata kipato cha uhakika.
“Mazungumzo na Viongozi hao sio tu kuimarisha mahusiano na viongozi bali hata wananchi wa kawaida ambao ni makundi ya vijana na wanawake kwa kuwajengea uwezo wa kuwapa mafunzo ya ujasiriamali,ufundi,kilimo na uvuvi.
Zanzibar ni moja ya nchi inayonufaika na mafunzo ya kilimo cha umwagiliaji kutoka nchini Vietnam, ambapo wakulima wengi wamekuwa wakifanya kilimo hicho na kujipatia mpunga mwingi”, alisema.
Katika maelezo yake Dk.Mabodi, alisema falsafa ya kutangaza utalii Kimataifa ya Royal Tour imeleta matokeo chanya kwa nchini mbali mbali Duniani kuonyesha dhamira ya kuja kutalii na kuwekeza nchini.
Sambamba na hayo Dk. Mabodi, amesema masuala mengine yaliyojadiliwa kwa kina ni pamoja na CPV kutoa fursa ya mafunzo ya uongozi kwa makada wa CCM Zanzibar sambamba na ufadhili wa masomo kwa Vijana wa CCM Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu huyo, alitaja mambo mengine yaliyosisitizwa kuwa ni pamoja na nafasi ya kubadilishana uzoefu kwa watendaji wa CCM na CPV sambamba na uwekezaji wa pamoja wa vyama hivyo kwenye miradi ya kiuchumi,kilimo na uimarishaji wa Vyuo vya Makada wa CCM.