Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deo Ndejembi amefunga mafunzo ya awali kwa maafisa uchunguzi na maafisa uchunguzi wasaidizi wa TAKUKURU 536. Mafunzo hayo yalifanyika katika Chuo Cha Polisi CCP Moshi. Maafisa hao walikua mafunzoni kwa takribani miezi mitano.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo Naibu Waziri Ndejembi amewataka maafisa hao kwenda kufanya kazi kwa weledi, Uadilifu na kutanguliza uzalendo mbele ili kulinda imani ya wananchi kwa Serikali yao.
” Niwasihi nyote ambao mmehitimu mafunzo haya kwenda kufanya kazi kwa uadilifu, Serikali chini ya Rais Samia imewekeza fedha nyingi katika kutekeleza miradi ya maendeleo hivyo ni jukumu lenu kama maafisa uchunguzi kuhakikisha hakuna fedha yeyote ya Serikali inapotea kwenye miradi hiyo.
Serikali imewaamini mafunzo haya yamegharimu takribani Sh Bilioni 2, lakini pia hatutegemei kuona baada ya kuanza kazi na kupangiwa vituo vyenu vya kazi mnaanza kuomba uhamisho, niagize hapa hakuna afisa yeyote ambaye atahamishwa kwenye kituo alichopangiwa kazi hadi baada ya Miaka mitano,” Naibu Waziri Ndejembi.