Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
VIKUNDI vya ujasiriamali Wilayani Kibaha vimetakiwa kuwakatia bima za maisha wanachama wao ili wanufaike wakati wakipata majanga mbalimbali.
Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kibaha Mjini Amina Makona wakati wa sherehe za miaka mitano ya kikundi cha wanawake cha Super Women 2017.
Makona alieleza ,bima ya maisha ni muhimu kwa vikundi zinapotokea changamoto mbalimbali bima hizo huwasaidia wanachama kwani wanakuwa hawana uwezo wa kuendelea kufanya shughuli zao.
“Kuwakatia bima za maisha wanachama ni jambo zuri sana na linapaswa kufanya na vikundi vingine ili bima hiyo isaidie kwenye changamoto mbalimbali zikiwemo za kufiwa, ugonjwa, uzazi na nyinginezo,”alisema Makona.
Katibu wa kikundi hicho Meri Msimbe alisema kuwa malengo ya Super Women 2017 ni kukopeshana kwa riba nafuu ili kuinuana na kusaidia makundi maalumu.
Naye mlezi wa kikundi hicho Elizabeth Msimbe ambaye pia ni mwalimu wa ujasiriamali alisema kuwa ili kikundi kiweze kufanya vizuri lazima kifuate katiba.
Msimbe alisema kuwa pia wajasiriamali wanapaswa kuzingatia muda na kuacha kuingiza masuala binafsi kwenye kikundi na kuwa na mshikamano na ushirikiano.