Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam.
Uchaguzi mkuu wa chama cha gofu Tanzania (TGU) umepamba moto baada ya mchezaji maarufu wa klabu ya Lugalo, Gilman Kasiga amechukua fomu kuwania nafasi ya uenyekiti.
TGU itachagua viongozi wake umepangwa kufanyika Oktoba 6 kwenye klabu ya Gymkhana ya mkoani Morogoro ambapo Oktoba 5 itakuwa siku ya mchujo wa wagombea.
Pia mchezaji wa timu ya gofu ya Arusha Gymkhana Pridence Kamugisha Kaijage naye amechukua fomu ya kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu ya kugomea uongozi, Kasiga alisema kuwa sababu kubwa ya kuwania nafasi hiyo ni kuleta maendeleo makubwa ya mchezo huo hapa nchini akianisha maeneo makuu matatu.
Kasiga alisema kuwa eneo la kwanza ni kuendeleza mchezo wa gofu kwa vijana ili kuwa na ‘mastaa’ wajao mara baada ya kizazi kilichopo kuacha kucheza na pili kuwazesha watu wazima kujiunga na mchezo ikiwa sehemu ya kuhimarisha mtandao miongoni mwao.
“Lengo la tatu ni kuhimarisha wachezaji wa gofu wa kulipwa ambao kimsingi ndio makocha wa wachezaji wa sasa, vijana na watu wazima. Alisema kuwa uongozi wake utazingatia msingi yote ya utawala bora ikiwa pamoja na uadilifu , uwazi, nidhamu na masuala mbalimbali ambayo yatawavutia wadau ikiwa pamoja na makampuni kudhamini mashindano mbalimbali,” alisema Kasiga.
Alisema kuwa wanatarajia kuwa na mafunzo mbalimbali ya ufundi kwa wachezaji kwa lengo la kuboresha zaidi viwango vya wachezaji. Alifafanua kuwa kutakuwa na mipango ya maendeleo ya muda mfupi, kati na mrefu ili kufingia kiwango cha juu kabisa cha maendeleo.
“Pia tutauleta mchezo wa gofu kwa jamii yote ya Watanzania na kuondoa dhana ya mchezo kuwa ni wa watu wenye kipato cha hali ya juu (matajiri), jambo ambalo limewafanya wachezaji chipukizi wenye vipaji kuogopa kucheza, vijana wenye rika la kushindana na watu wazima kushindwa kuingia,” alisema Kasiga.