Mkuu wa Ushirikishwaji wa Jamii Nchini Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Engelbert Kiondo akimpa zawadi mojawapo ya Mwanafunzi aliyefanya vizuri katika mitihani kwenye sherehe ya mahafali ya darasa la saba ya shule ya msingi Tumaini Mission Trust iliyopo mkoani Arusha Septemba 17, 2022.
Mkuu wa Ushirikishwaji wa Jamii Nchini Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Engelbert Kiondo akimkabidhi kitabu cha muongozo wa kuzuia na kufichua uhalifu Mkuu wa Shule ya msingi Tumaini Mission Trust Bi. Namnyaki Mollel katika mahafali ya darasa la saba yaliyofanyika katika shule hiyo iliyopo mkoani Arusha Septemba 17, 2022.
********************
Na. Gasto Kwirini Jeshi la Polisi Arusha.
Jeshi la Polisi limesema chanzo cha matukio mengi ya uhalifu yaliyojitokeza nchini hivi karibuni hasa kwa vijana wenye umri chini ya miaka 18 kumetokana na wazazi kuacha majukumu yao ya malezi kwa watoto wao, hali inayopelekea kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili katika jamii na kusababisha kuibuka kwa vitendo hivyo vya kihalifu.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Ushirikishwaji wa Jamii Nchini Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Engelbert Kiondo jana jioni wakati akizungumza na wazazi pamoja na watoto akiwa mgeni rasmi katika mahafali ya darasa la saba ya shule ya msingi Tumaini Mission Trust iliyopo mkoani Arusha.
Alisema kutokana na kushindwa huko kwa wazazi kwenye malezi kumepelekea watoto kuacha kuwaheshimu na kuwatii wazazi, viongozi ama sheria za nchi na wengine wanafika mbali zaidi na kutishia jamii pamoja na viongozi wa Serikali akitolea mfano ‘‘Panya road’’ ambao wamefanya matukio ya kihalifu katika Jiji la Dar es Salaam.
SACP Kiondo alibainisha kuwa ni wakati sasa kwa jamii kuchukua jukumu lake la malezi bora kwa watoto wao ambapo alisema Jeshi la Polisi limekuja programu maalumu ya kukaa na wazazi, waalimu pamoja na kamati za shule kwa ajili ya kufuatilia tabia za mtoto mmoja mmoja hali ambayo itasaidia kuwarudisha watoto kwenye maadili mema.
Sambamba na hilo pia alisema jeshi hilo kupitia Polisi Kata ambao wamepangwa katika kata zote kwa ajili ya kufuatilia changamoto za uhalifu pamoja na kutoa elimu za masuala ya usalama litaendelea kutoa ushirikiano kwa jamii hali ambayo itasaidia kujua tabia za watoto wanaojihusisha na uhalifu.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo alisema Jeshi la Polisi mkoani humo limekua likitoa elimu ya usalama kwa shule zote kuanzia Msingi hadi Vyuo Vikuu ambapo alibainisha kuwa Askari wamekua wakifika katika shule na vyuo mbalimbali kwa lengo la kuwafundisha masuala ya usalama ikiwemo ukatili wa kijinsia pamoja na mambo mengine ya kihalifu.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo Bi. Namnyaki Mollel alisema malezi ya watoto kitaaluma na kitabia yanatagemea pande mbili, hivyo akatoa wito kwa wazazi au walezi kushirikiana pamoja na walimu katika malezi na makuzi ya watoto wao na kutowaachia Walimu pekee.