Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akivuna nyanya katika Kitalu nyumba kinachohudumiwa na vijana waliopata mafunzo ya Kilimo cha Kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba ambayo yametolewa na Ofisi hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akiongea na Vijana wanaolima Kilimo cha Kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba baada ya kupata mafunzo hayo yaliyotolewa na Ofisi hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Jerry Muro.
****************************
Na: Mwandishi Wetu – Singida
Vijana zaidi ya 12,000 katika halmashauri 117 Mikoa 17 wamenufaika na mafunzo ya Kilimo cha Kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba.Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imetoa mafunzo hayo ili vijana waweze kujiajiri, kuajiri wenzao na kujipatia kipato kupitia sekta ya kilimo.
Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imetenga Shilingi. Bilioni 1.3 kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo kwa vijana 2,400 kutoka katika halmashauri 24 nchini.
Amesema hayo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako wakati wa ziara yake mkoani Singida yenye lengo la kukagua maendeleo ya Mafunzo hayo ya kilimo cha kisasa yanayotolewa kwa vijana.
Amesema kuwa, Rais Samia anathamini vijana na ndio maana amekuwa akitoa maelekezo ya kubuni miradi ambayo itawakwamua vijana kimaisha na kiuchumi kwa kuwapatia ujuzi utakao wasaidia waondokane na changamoto ya ajira kwa kujiajiri na kuajiri wenzao kupitia ujuzi waliopatiwa.
“Niwahakikishie vijana serikali anayoiongoza Mhe. Rais, Samia imekuwa mstari wa mbele katika kushughulikia masuala ya vijana ikiwemo kuwapatia mafunzo ya kuwapatia ujuzi wa stadi zitakazo wawezesha kujiajiri ili kuimarisha kipato chao,” amesema
“Mhe. Rais Samia katika mwaka wa fedha 2022/23 ameamua kuongeza bajeti ya kilimo kutoka bilioni 250 hadi bilioni 990. Mhe. Rais pia ametoa ruzuku ya mbolea hivyo tunategemea vijana wengi kuchangamkia fursa hii kwa kuhiriki katika kilimo biashara”
Mhe Waziri Ndalichako amezitaka halmashauri kuendelea kujenga vitalu nyumba katika ngazi za kila Tarafa ili vijana wengi wapate ajira kupitia kilimo.Aidha, amesisitiza uhamasishaji wa Watu wenye Ulemavu kwenye Kilimo cha Kitalu nyumba kwa kuwa kilimo hicho hutumia teknolojia zaidi kuliko nguvu hivyo kupitia kilimo hicho wataweza kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mhe. Jerry Muro ameahidi kusimamia ipasavyo mradi huo ambapo amaeeleza kuwa wiliaya hiyo imepanga kujenga vitalu nyumba kwenye tarafa 4 ili kuwezesha vijana kushiriki kwa wingi katika kilimo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti vijana walionufaika na mafunzo hayo wamesema kuwa mafunzo hayo yamekuwa chachu ya maendeleo kwa kuwa wanao uhakika wakupata kipato kutokana na kujifunza njia bora za kilimo ambacho kinawawezesha kulima kwa tija.