**************************
Na Mwandishi wetu
UMOJA wa Wanahabari Wanawake chini ya Asasi ya Sauti ya Matumaini (SUMAF) umetoa msaada wa taulo za kike 600 kwa wanafunzi 100 viziwi wa Shule ya Msingi Buguruni Viziwi jijini Dar es Salaam.
Lengo la msaada huo ni kuungana mkono juhudi za serikali kutoa elimu bure katika kulisaidia kundi la wenye ulemavu ambao wanashindwa kusoma kutokana na kukosa baadhi ya mahitaji.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa SUMAF, Mary Geofrey, alisema kupitia msaada huo kila mwanafunzi wa kike katika shule hiyo, alipata pakiti sita atakazotumia kwa miezi sita.
Mary alisema wanaamini msaada huo utawafanya wanafunzi kuwa nadhifu, kuwaongezea tabasamu, kujiamini na ari ya kupenda masomo itakayochochea na kuongeza ufaulu wao.
“Mradi wetu huu tulianza na shule mbili wilayani Temeke, ambazo ni Shule ya Msingi Jeshi la Wokovu na Mtoni Maalum na jumla ya wanafunzi 100, tuliwafikia na kuwapatia taulo za kike 1,000 pamoja na elimu ya kujitambua na kujithamini.
“Malengo ya asisi yetu ni kufikia wanafunzi wengi zaidi wenye ulemavu wa aina mbalimbali kote nchini katika kuhakikisha tunawapa tabasamu ili wajione nao wanathaminika katika jamii,” alisema Mary.
Aidha, alisisitiza kuwa SUMAF ni umoja wa Wanahabari Wanawake, walioamua kujitoa kurudisha tabasamu kwa jamii kwa njia ya vitendo, badala ya kutumia kalamu peke yake huku wakiwa na Kauli mbiu ya ‘Nilinde ithamini Kesho Yangu’.
Naye Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAF, Penina Malundo, alisema umoja wao upo chini ya asasi hiyo inayoendelea kupigania haki ya mtoto wa kike mwenye ulemavu katika maeneo mbalimbali hususani kwenye masuala ya afya ya uzazi, kujitambua pamoja na ukatili wa kijinsia.
Alisema mradi huo unafanyika chini ya kampeni yake yenye kauli mbiu ya Ithamini na Ilinde kesho yangu na wanaratajia kuwafikia watoto wengi zaidi wenye ulemavu waliopo kwenye maeneo mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam.
“Kwa hivi karibuni tunatarajia kuwafikia watoto wengine wenye ulemavu katika Shule ya Msingi Maweni, Kigamboni, Mjimwema pamoja na Kituo cha Amani Centre na Mihayo vilivyopo mkoani Morogoro,” alisema Penina
Awali akikabidhi taulo hizo kwa watoto hao kwa niaba ya Mbunge wa Viti Maalum, mkoa wa Dar es Salaam, Janeth Masaburi, Diwani wa Viti Maalum Dar es Salaam, Beatrice Nyamisango, alisema amefurahishwa na kitendo cha Wanahabari hao kujitoka kwa lengo la kuwasaidia wenye uhitaji hasa walemavu.
“Hakika nimefurahi kuwaona wadada wameamua kujitoka kwa hali na mali kuwasaidia wengine, Mungu awabariki na kuwaongezea mara dufu pale mlipopunguza,” alisema Nyamisango
Naye Mwakilishi Kutoka Kampuni ya Shree Jalaram Seve Mandal, Said Nassoro alisema taasisi yao imekuwa ikiendelea kusaidia kundi la wahitaji mbalimbali kwa kuwapatia misaada kwa lengo la kuhakikisha inarudisha furaha kwao.
Ailisema kampuni yao inatoa misaada mingi katika jamii ikiwamo katika Kituo cha Watoto Yatima Chamanzi Mbagala, matibabu ya shida ya ngiri maji ,kutoa wheelchair kwa walemavu mbalimbali wa viungo.
“Tunashukuru kuungana na umoja wa waandishi wa habari Dar es Salaam katika kuadhimisha siku ya viziwi duniani shule ya msingi viziwi na kuwapatia taulo za kike 600 kwa lengo la kuwasaidia kujistiri katika mzunguko wao wa hedhiwanapoingia
Mbali na vitu vingine pia taasisi imetoa zawadi mbalimbali kama maji, Juice, biskuti pamoja na chakula katika kusherekea siku hiyo.