Msemaji wa Yanga Haji Manara,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Septemba 18,2022 jijini Dodoma
…………………………………….
Na Alex Sonna-DODOMA
MSEMAJI wa Yanga Haji Manara amesema kuwa hausiki kuzuia mchakato wa Yanga kupata Afisa Habari mpya kwani yeye bado amejiriwa na anakula mshahara wake vizuri.
Kauli hiyo ameitoa leo Septemba 18,2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari Manara ambaye kwa sasa amefungiwa miaka miwili na TFF kujihusisha masuala ya soka amesema yeye hausiki kuzuia mchakato huo wala watu wasimsingizie.
“Mimi sizuii Afisa Habari mpya kuja Yanga,sijapata nguvu hiyo msinisingizie mimi bado nimeajiriwa Yanga nalipwa mshahara wangu vizuri,”amesema Manara.
Manara amesema yeye amehusika kumsaidia mchambuzi Ally Kamwe kupata ajira Azam iweje leo tena awe mbaya.
“Nimemsaidia lakini ananisema kwenye mitandao ya kijamii alafu nikae kimya mimi sio mnafiki kwanza dini yangu inanikataza yaani yeye awe na haki lakini yeye hataki kukosolewa mambo ya Januari kwanini ayalete leo,”amehoji Manara
Amesema aliyoyasema Kamwe hayana ukweli wowote kwamba anazuia ajira yake Yanga na ameshangaa kumzungumzia vibaya katika interview.
“Anasema nilimkatalia salamu tulipokutana Zanzibar sasa ningewezaje kuwa mnafiki kwa mtu aliyenitukania binti yangu kwanza hata Mwenyezimungu hapendi ni dhambi,”amesema.
Kuhusu adhabu ya kufungiwa na TFF miaka miwili Manara amesema ameikubali na anaendelea kuitumikia huku akidai mambo mengine waachiwe kamati ya rufaa na wanasheria.