Na .Zillipa Joseph, Katavi
Jumla ya wanafunzi 471 wa darasa la kwanza na la awali wa mtaa wa Tulieni katika kata ya Nsemulwa katika Manispaa ya Mpanda wameepukana na adha ya kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita nane kwa siku kufuata elimu katika shule ya msingi Nsemulwa baada ya shule shikizi ya Tulieni kuanza kutumika.
Shule hiyo shikizi ya Tulieni ina jumla ya vyumba vine vya madarasa na ofisi moja ya walimu.
Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na mwandishi wa habari hizi akiwemo Anastazia Mwanakatwe na Stella Joseph wa darasa la kwanza wanasema wanafurahi kuwepo shuleni.
Mwalimu Alexandra Semi ni mmoja wa walimu wanaofundisha katika shule shikizi ya Tulieni, amesema wako walimu wawili na mwalimu mwingine anaitwa Adolf Kayoka.
Mwalimu Semi ametaja changamoto za shule hiyo kuwa ni pamoja na kuwa na mtundu machache ya vyoo ambapo yapo matundu yapo manne tu, upungufu wa samani kama madawati kwa wanafunzi, meza, viti, na makabati katika ofisi ya walimu huku changamoto kubwa kabisa ikiwa ni kukosekana kwa huduma ya maji.
Alisema hali hiyo inawafanya kuwaagiza watoto kuja na maji shule ambayo hata hivyo hayatoshelezi usafi kutokana na ukweli kwamba maji wanayobeba ni kwenye chupa tu na yanaishia kusaidia mwanafunzi kunywa.
Aidha bado hawajaanza utaratibu wa kuwapikia watoto chakula shule kutokana na mazingira magumu yaliyopo hapo shuleni.
Mwalimu Said Mbogo ni mwalimu mkuu katika shule ya msingi Nsemulwa ambaye pia anasimamia shule shikizi ya Tulieni anasema licha ya kufunguliwa kwa shule hiyo bado ina changamoto kadhaa na kuomba wadu mbali mbali kujitokeza kuisaidia kukamilika na hatimaye isajiliwe na kuwa shule ya msingi Tulieni.
Mwl. Mbogo alisema mtaa wa Tulieni unaendelea kuongezeka watu wanaojenga na kuishi maeneo hayo hali inayoashiria kuwa ni lazima kuwepo na shule kwa ajili ya kuhudumia wanafunzi.
Aliwataka watu wenye mapenzi mema kujitolea kwa hiari kuchangia ujenzi wa shule hiyo.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Tulieni wamesema shule hiyo imesaidia kuinua mwamko wa wazazi kuwaaandikisha watoto shule kwani kwa kutegemea shule ya Nsemulwa peke yake ilikuwa ni vigumu kutokana na umbali uliopo hasa kwa watoto wadogo.