Na John Walter-Babati
Jamii imetakiwa kuacha tabia ya kuwaficha ndani watoto wenye ulemavu ili wapate haki wanazostahili.
Wapo baadhi ya watu Kwenye jamii hushindwa kuwapa hadhi wanayostahili watu wenye ulemavu na kuwatenga pamoja na kuwaficha ndani hali inayosababisha kukosa haki zao.
Akizungumza mjini Babati katika uwanja wa mpira wa Kwaraa kwenye Michuano maalum kuelekea siku ya watu wasioona maarufu kama Fimbo nyeupe inayoendelea, Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya mji wa Babati Anna Fissoo ameitaka jamii kutoa taarifa kwa viongozi wa mitaa au vijiji juu ya vitendo vinavyokwamisha ustawi kwa watu wenye ulemavu ili wapate msaada.
“Mtu akiwa na mtoto ambaye ana tatizo la kutokuona,msiwafiche wanahitaji huduma kama walivyo watoto wengine, lakini tuwatambue na kuwaheshimu, tuheshimu utu wao”
Ni siku maalumu ambayo huadhimishwa kote ulimwenguni kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa macho (hasa wale waliopoteza uoni, yaani wasioona).Fimbo nyeupe, ni fimbo maalumu inayotumika na mtu asiyeona, ilikumtambulisha kwa watumiaji wengine wa barabara , wakati wowote na hasa anapokuwa akitembea.
Siku ya watu wasioona itafanyika Oktoba 21,2022 kitaifa mjini Babati mkoa wa Manyara ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa.
Lengo la maadhimisho ya siku hii, ni kuihamasisha jamii na watumiaji wote wa barabara kama vile madereva, kuiheshimu fimbo nyeupe na kumsaidia asiyeona anapotembea na anapovuka barabara.
Pia siku hii hutumika kutambulisha shughuli mbalimbali zinazofanywa na wasioona, malengo yao, mahitaji yao, uwezo wao katika suala zima la maendeleo, changamoto wanazokabiliana nazo, na mchango unaohitajika toka Serikalini na wadau wengine wa maendeleo.
Katika mchezo huo uliochezwa Septemba 16,2022, uliwakutanisha Bajaji Fc Vs Maisaka Star ambapo dakika 90 katika uwanja wa Kwaraa ubao ulisoma Bajaji Fc 3-2 Maisaka Star.