Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema Serikali imeendelea kutekeleza wajibu wa kulinda haki za binadamu na watu kwa kutekeleza Sheria, Sera, Mipango, Mikakati na programu zinazotafsiri upatikanaji wa haki mbalimbali.
Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora leo Septemba 15, 2022 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma.
‘’Serikali imeendelea kutekeleza wajibu wa kulinda haki za binadamu na watu kwa kutekeleza Sheria, Sera, Mipango, Mikakati na programu zinazotafsiri upatikanaji wa haki mbalimbali kama vile haki ya afya na mazingira bora; haki ya kupata elimu; haki ya maendeleo na haki ya kumiliki mali’’ amesema Dkt. Ndumbaro.
Dkt. Ndumbaro aliongeza ‘’kuhusu haki ya afya Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya vilivyosajiliwa imekuwa ikiongezeka. Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi, 2022, vituo hivyo vimeongezeka kufikia 8,549 ikilinganishwa na vituo 8,458 mwaka 2020’’.
Pia kwa upande wa haki za kiuchumi Dkt. Ndumbaro amesema Serikali inatekeleza vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026). Vipaumbele hivyo vinajumuisha kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, kukuza biashara na uwekezaji, kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu. Mpango Kazi huu unatambua haki za binadamu kama msingi wa kuleta maendeleo ya kudumu.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Mkondo amesema uwepo wa Tume hii ni ishara kuwa Serikali imeweka umuhimu katika masuala ya Utawala Bora katika ngazi zote za uongozi wa Taifa letu kama changamoto za utawala bora zikitatuliwa matatizo mengi kama vile rushwa, utawala wenye upendeleo na unyanyasaji wa wafanyakazi yatapungua na hatimae kuisha.
Bi. Makondo aliongeza, ‘’utayari wa Serikali kuwa na chombo kama Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kinachopima na kuishauri Serikali kwenye utendaji kazi wake wa kulinda na kukuza haki za binadamu ni ushahidi kuwa Tanzania ni nchi inayothamini demokrasia na kuwa ina Serikali ambayo iko tayari kuwajibika kwa chombo kama hiki chenye sifa ya uchunguzi.’’
Vilevile, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Mhe. Mathew Maimu wakati akimkaribisha Dkt. Ndumbaro ambaye ndiye aliyekuwa Mgeni Rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo amesema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita hali ya Haki za Binadamu imeimarika na Tume imetekeleza majukumu yake kwa uhuru.
Aidha, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala imempatia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Tuzo Kwa kutambua mchango wake katika kutetea na kuimarisha Haki za Binadamu na Misingi ya Utawala Bora. Tuzo hiyo imepokelewa na Waziri Ndumbaro kwa niaba ya Rais.