Naibu Waziri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga amesema utoaji wa chakula na lishe kwa wanafunzi wakiwa shule ni suala muhimu kwa kuwa upo uhusiano mkubwa kati ya afya ya mwanafunzi na maendeleo yake kitaaluma.
Mhe. Kipanga amesema hayo jijini Dodoma katika hafla ya utiaji saini kujiunga na muungano wa chakula shuleni ambapo amesema mwanafunzi anapokosa chakula shuleni hukosa usikivu wakati wa ujifunzaji, mahudhurio hafifu, utoro wa rejareja na hata kukatisha masomo.
Ameongeza kuwa pamoja na jitihada za Serikali katika kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, upatikanaji wa matokeo mazuri ya elimu hutegemea afya aliyonayo mwanafunzi.
“Mwezi Oktoba, 2021 Wizara yangu ilizindua Mwongozo wa Kitaifa wa Utoaji wa Huduma ya Chakula na Lishe kwa Wanafunzi wa Elimumsingi ili kuweka utaratibu wa kitaifa ambao utawezesha wanafunzi kupata huduma hiyo muhimu. Naishuruku OR-TAMISEMI kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa mwongozo huu katika mikoa na Halmashauri zote nchini”, amesema Mhe Kipanga.
Akizungumzia kujiunga na muungano wa chakula shuleni ambao leo Serikali kupita Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetia saini fomu ya kujiunga na muungano huo Naibu Waziri Kipanga amesema lengo ni kumwezesha kila mwanafunzi kupata lishe bora, afya na elimu.
Aliongeza kuwa pamoja na kuwezesha wanafunzi kupata lishe shuleni utatuwezesha kupata uzoefu wa namna nzuri ya kutekeleza mpango wa chakula shuleni kwa kushirikisha jamii kwani muungano huo ni kundi la kimataifa linalojumuisha nchi mbalimbali duniani, mashirika ya kiraia, wasomi na sekta binafsi.
“Kujiunga na muungano huu kutawezesha wadau wetu wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali, Makampuni binafsi pamoja na vyombo vya Habari, kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa chakula na lishe shuleni,” amesema Mhe. Kipanga.
Ametaja nchi za Afrika ambazo tayari zipo kwenye muungano huo kuwa ni Angola, Benin, Burkina Faso, Burundi, Kamerun, Chad, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Misri, Ethiopia, Gambia, Guinea, Kenya, Lesotho, Liberia, Madagasca, Mali, Maurtania, Morocco, Msumbiji, Namibia, Niger, Jamhuri ya Kongo, Rwanda, Senegal, Somalia na Sudan.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani Sarah Gordon- Gibson ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kujiunga na kuwa washirika wa muungano wa chakula shuleni kwani kwa kufanya hivyo ni kuwekeza kwa watoto wetu ambao ndio taifa la kesho.
Kwa upande wake mwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Suzan Nusu amesema tukio la kutia saini kujiunga na muungano wa chakula Shuleni limeonesha dhamira ya dhati ya Serikali kuhakiksha watoto wote wanapata chakula shuleni na kwamba wanahidi kusimamia utekelezaji wake ili watoto wasome bila changamoto zozote.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanafunzi mbalimbali wa shule za Msingi na Sekondari za Mkoani Dodoma ambao wameshiriki katika hafla hiyo wameipongeza Serikali kwa kujiunga na muungano wa Chakula Shuleni kwani utawawezesha kupata chakula shuleni na kuwaepusha na vishawishi vinavyoweza kukatisha ndoto zao za kupata elimu.