*******************
Mnamo tarehe 14/09/2022 majira ya saa 07:45 mchana huko pipeline – Tazama, Wilaya ya Mbeya Vijijini katika barabara ya Mbeya – Njombe, Gari yenye namba T.391 AFT Scania ikiendeshwa na dereva AHAMED OMARY @ MUBA, [25] Mkazi wa kurasini Dar es Salaam mali ya makata husein @ kibacha mkazi wa Tabata – Dar es salaam ikitokea nchini Congo kuelekea Dar es salaam iligonga kwa nyuma Gari namba SM 14279 Toyota land cruiser Prado iliyokuwa inaendeshwa na ALEX MTABIKA [48] Dereva wa Halmashauri ya Igunga – Tabora, kisha kugonga Gari namba T.823 DKT / T.610 CFH Howo – Tenker ikiwa tupu mali ya kampuni ya lake oil ikiendeshwa na HAMAD ALMAS @ ATHUMAN [29] Mkazi wa Dar es salaam zote zikiwa uelekeo mmoja kisha kugonga Gari namba PE. 7097 / PE. 7078 IVECO ya nchini Malawi iliyokuwa inaendeshwa na PETER AMAN @ JALI [50] Mkazi wa Lilongwe nchini Malawi iliyokuwa ikitokea Dar es salaam kuelekea Malawi ikiwa na mafuta (Petroleum) na kusababisha vifo kwa watu watatu wanaume wawili na mwanamke mmoja ambao ni:-
- ALEX MTABIKA [48] Dereva wa SM 14279, Halmashauri ya Igunga-Tabora, 2. FATUMA OMARI LATU [44], Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Igunga – Tabora na
- SHAFII SAID [27] Mkazi wa Buguruni malapa – Dar es salaam, utingo wa gari T. 391 Scania.
Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva kushindwa kulimudu gari likiwa kwenye mteremko mkali kisha gari hilo kuyagonga magari matatu. Aidha dereva wa Gari SM 14279 halmashauri ya Igunga-Tabora kukaidi amri halali ya askari wa usalama barabarani kusubiri kwanza malori kupita kutokana na utaratibu wa kupitisha magari kwa awamu katika eneo hilo lenye mteremko mkali. Dereva wa Gari namba T.391 AFT Scania AHAMED OMARY @ MUBA [25] Mkazi wa kurasini Dar es Salaam anashikiliwa na Jeshi la Polisi.
Sambamba na hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mh. Juma Homera amefungua rasmi barabara ya mchepuo [By Pass] eneo la Inyala ambayo kwa sasa itakuwa ikitumika kupitisha magari ya abiria na magari madogo huku barabara ya zamani ya lami itatumika kupitisha magari makubwa ya mizigo. Lengo na kuepusha magari ya mizigo na abiria kutopishana katika eneo la Inyala Pipeline lenye mteremko mkali ambalo limekuwa hatarishi na kupelekea ajali za mara kwa mara.
WATU WANNE WA FAMILIA MOJA WAKUTWA WAMEFARIKI DUNIA.
Ni kwamba mnamo tarehe 13.09.2022 majira ya saa 07:30 mchana huko kwenye nyumba moja iliyopo Kitongoji cha Kibumbe, Kijiji cha Ibula, Kata ya Kiwira, Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya iligundulika kuwa kuna miili ya watu wanne wa familia moja wamefariki dunia ndani ya nyumba hiyo huku milango yote ya nyumba hiyo ikiwa imefungwa kwa ndani.
Baada ya kuvunjwa mlango na kuingia ndani ilikutwa miili minne ya wanafamilia moja ikiwa imeharibika vibaya na inasemekana imekaa zaidi ya mwezi mmoja. Miili hiyo imetambulika kuwa ni:-
- SAIMON OSCAR MTAMBO [41] Mwalimu wa Shule ya awali na msingi Mbuja,
- FORTUNATA GEORGE ABRAHAM [38] Mwalimu Shule ya msingi Ikuti,
- OSCAR SAIMON MTAMBO [14] Mwanafunzi kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Busokelo na
- FROLENCE SAIMON MTAMBO [09] Mwanafunzi Darasa la nne Shule ya msingi Ikuti.
Chanzo cha tukio hili kinachunguzwa ili kubaini kiini cha tukio na aliyehusika/waliohusika. Miili ya marehemu imefanyiwa uchunguzi na daktari na imehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Rungwe.
AJALI YA MOTO KUUNGUZA BWENI.
Ni kwamba mnamo tarehe 13.09.2022 majira ya saa 01:40 usiku huko katika Shule ya Sekondari Mwakaleli iliyopo Kata ya Luteba, Tarafa ya Busokelo, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya, Bweni la wasichana liitwalo Mwantimwa liliteketea kwa moto na kuunguza samani zote zilizokuwa ndani ya bweni hilo.
Bweni hilo lilikuwa linatumiwa na wanafunzi 136 likiwa na vitanda 68. Katika tukio hilo pesa taslimu za wanafunzi shilingi 2,020,000/=, madaftari, nguo mbalimbali za wanafunzi zenye thamani ya shilingi 32,027,500/= viliungua, mali za shule vitanda 68, magodoro 136, unga wa sembe kilo 5,100, chumvi kilo 420, mchele kilo 840, sukari kilo 180, mafuta ya alizeti lita 420 vyote vikiwa na thamani ya shilingi 18,006,000/= viliteketea kwa moto hivyo kufanya jumla ya thamani ya mali zote zilizoteketea kwa moto kuwa na thamani ya shilingi 52,053,500/=.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya tumefanya uchunguzi na kubaini chanzo cha moto ni kwamba mwanafunzi JACKLINE CHARLES [14] alikwenda bwenini akiwa na kiberiti wakati wanafunzi wengine wakiwa darasani na kuchoma moto godoro moja na kuondoka. Pia mwanafunzi wa kidato cha pili SALLOM MAHMOUD [15] anashikiliwa kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo.