Na Samir Salum, Lango la Habari
Uongozi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kishapu umeushukuru Mgodi wa Almasi wa Mwadui Williamson Diamond Ltd uliopo Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga kwa kutoa misaada mbalimbali ikiwemo kujenga uzio wa shule hiyo.
Akisoma risala ya shukrani mara baada ya kutembelewa na uongozi wa mgodi huo jumanne September 14, 2022, Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kishapu Mwalimu Segeleti Masanja ameeleza kuwa shule hiyo ilikuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa uzio hali iliyokuwa ikihatarisha usalama wa wanafunzi, kutokuwa na Maabara kwa ajili ya kujifunzia kwa vitendo na pia ukosefu wa makaro ya kuoshea vyombo na kufulia.
Amesema kuwa Shule iliwasilisha changamoto hizo kwa uongozi wa Mgodi wa Almasi wa Mwadui Williamson Diamond Ltd mnamo April 04, 2022 ambapo zilianza kufanyiwa kazi na hadi sasa tayari shule ina uzio hivyo usalama wa shule na wanafunzi kuimarika, pia uwepo wa meza 10 za maabara zitakazowasaidia kusoma masomo ya sayansi kwa vitendo pamoja na makaro ya kuoshea vyombo na kufulia nguo.
“tunawashukuru sana kwa msaada mlioutoa kwa ajili ya kuisaidia shule hii mpaka sasa uzio umekamilika hivyo usalama wa shule umeimarika na wanafunzi wanaishi kwa amani tofauti na awali, meza za maabara zitawasaidia wanafunzi kusoma kwa vitendo na kwa ufanisi, kututengenezea makaro ya kuoshea vyombo na kufulia kutasaidia utunzaji wa mazingira ” ameeleza Makamu Mkuu wa Shule hiyo
Kwa upande wake Meneja mahusiano ya jamii wa Mgodi wa Williamson Diamond Ltd Bernard Mihayo ameeleza kuwa msaada huo uliotolewa na mgodi umegharimu shilingi milioni 18 na kuongeza kuwa bado changamoto nyingine zinaendelea kutatuliwa ikiwemo kujenga jiko la muda ili kuwa na mazingira mazuri kwa ajili ya kuandaa chakula cha wanafunzi hao.
Mihayo ameeleza kuwa lengo la kutoa misaada shuleni hapo ni kuhakikisha watoto hasa wa kike wanapata elimu ili kuondoa mila na desturi potofu zinazomnyima mtoto wa kike haki ya kusoma.
“Shule hii ilishawahi kuwa ya kwanza kiwilaya kwenye mitihani ya kidato cha pili na wanafunzi wanaonga kiingereza vizuri hali hii inatia moyo, hivyo niwasihi waendelee kusoma kwa bidii” amesisitiza
Aidha Meneja Mihayo alimkabidhi Mashine ya Kuchonga vyuma, mwalimu wa ufundi wa shule ya ufundi ya Sekondari Mwadui, John Mihumo mara baada ya kutoa msaada wa kuifanyia matengenezo baada ya kuharibika ambapo yamegharimu Shilingi milioni 4.
Akitoa Shukran mwalimu wa ufundi wa shule ya ufundi ya Sekondari Mwadui, John Mihumo amesema kuwa kuharibika kwa mashine hiyo kulisababisha wanafunzi kutosoma kwa vitendo hivyo baada ya matengenezo kutaleta matokeo chanya kwa kukuza uwezo wa wanafunzi katika uchongaji wa vyuma.