Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru akizungumza wakati wa kikao na Umoja wa Makampuni ya Huduma za Simu Tanzania (TAMNOA) ambapo walikutana kujadili changamoto na faida zilizopatikana kwa watoa huduma hao baada ya utekelezaji wa kukusanya tozo iliyoanzishwa na Serikali kilichofanyika jijini Dodoma.
Kamishna wa Sera wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Elijah Mwandumbya akizungumza wakati wa wakati wa kikao na Umoja wa Makampuni ya Huduma za Simu Tanzania (TAMNOA) ambapo walikutana kujadili changamoto na faida zilizopatikana kwa watoa huduma hao baada ya utekelezaji wa kukusanya tozo iliyoanzishwa na Serikali kilichofanyika jijini Dodoma.
Wajumbe wa kikao wakifuatilia wasilisho wakati wa kikao kati ya Serikali na ilichoongozwa na Umoja wa Makampuni ya Huduma za Simu Tanzania (TAMNOA) kilichoongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru, kilichofanyika jijini Dodoma.
(Picha na WFM – DODOMA)
*************************
Na Ramadhani Kissimba WFM -Dodoma
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imekutana na Umoja wa Makampuni ya Huduma za Simu Tanzania (TAMNOA) kujadiliana changamoto na faida zilizopatikana kwa watoa huduma hao baada ya utekelezaji wa kukusanya tozo iliyoanzishwa na Serikali.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru amesema madhumuni ya kikao hicho ni kusikia na kupata maoni ya watoa huduma hao kuhusu changamoto iliyojitokeza wakati wa utekelezaji wa tozo tangu zilipoanza hadi sasa.
Bw. Mafuru alisema Serikali imekuwa ikishirikiana na Makampuni ya simu tangu tozo hizi zilipoanzishwa ili kuwa na tozo ambazo sio mzigo sana kwa wananchi lakini zinatimiza lengo la Serikali la kupata Mapato kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo.
‘’Sote tumekubaliana na maelekezo tuliyopata kutoka Serikalini, kuwa Mhe. Rais ametuagiza tuangalie upya tozo hii na kuhakikisha kuwa tozo hii inabakia kuwa rafiki na haiwi mzigo kwa Watanzania’’ alisema Bw. Mafuru.
Bw. Mafuru aliongeza kuwa Serikali imekuwa na utamaduni wa kusikiliza maoni ya wananchi hivyo imeona ni muhimu kukutana na wadau wa Makampuni ya simu nchini ambao wana kundi kubwa la wateja wanaofikia milioni arobaini wanaofanya miamala ya kielektroniki kupitia simu.
Alisema kuwa pamoja na kuwa ukusanyaji wa tozo umeshaanza kutekelezwa lakini tayari Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na wataalamu kutoka katika sekta za simu na Benki wanafanya kazi kwa pamoja kuangalia namna ya kuwa na tozo bora ambayo itatimiza lengo lile lile la kumpa nafasi kila Mtanzania kuchangia maendeleo ya nchi yake lakini achangie kwa njia ambayo haimumizi na isiyokuwa na ukakasi.
Aidha, Naibu Mkurugenzi wa Halopesa, kutoka Halotel Tanzania, Bw. Magesa Wandwi aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwa Sikivu na kuendelea kupunguza kupunguza tozo katika vipindi tofauti hizo, tangu kuanzishwa kwake ambapo awali kulikuwa na punguzo la asilimia 30 katika mwaka 2021/2022 na katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali imepunguza tozo katika miala ya simu hadi kufikia asilimia 43.
Bw. Wandwi aliongeza kuwa punguzo hilo limerejesha kasi ya miamala ya simu ambayo ilipungua katika kipindi kilichopita.
Kikao hicho kilichoshirikisha makampuni ya simu za mkunoni ya Airtel, TTCL, VODACOM, TIGO na HALOTEL ni utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha tozo hizo hazimuumizi mwananchi.