KATIBU Tawala wa Mkoa wa Mtwara Abdalah Malela,akizungumza wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuzijengea uwezo Asasi za kiraia juu ya uelewa wa sheria na taratibu za uendeshaji wake leo Septemba 12,2022.
MWAKILISHI wa Mtandao wa Mashirika yasiyo ya kiserekali Mkoa wa Mtwara (MRENGO) Bw.Musfafa Kwiyunga,akizungumza wakati wa mafunzo ya siku mbili ya kuzijengea uwezo Asasi za kiraia juu ya uelewa wa sheria na taratibu za uendeshaji wake leo Septemba 12,2022.
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Mtwara Abdalah Malela,akiwa katika picha za pamoja mara baada ya kufungua mafunzo ya siku mbili ya kuzijengea uwezo Asasi za kiraia juu ya uelewa wa sheria na taratibu za uendeshaji wake leo Septemba 12,2022.
……………………………….
SERIKALI Mkoani Mtwara imesema kuwa inathamini mchango wa asasi za kiraia kutokana na umuhimu wa sekta hiyo katika kuchangia na kukuza maendeleo na ustawi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa Septemba 12, 2022 na Katibu Tawala wa mkoa wa Mtwara Abdalah Malela, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuzijengea uwezo Asasi za kiraia juu ya uelewa wa sheria na taratibu za uendeshaji wake.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Boma Mjini Mtwara, kwa usimamizi wa Taasisi ya Foundation For Civil Society yenye makao yake makuu Jijini Dar es salaam yakiwa yanalenga kujenga uwezo na kuhakikisha kuwa asasi za kiraia zinaelewa mahitaji ya kisheria katika kufanya kazi.
Vile vile yana lengo la kukumbushana wajibu wa serikali katika kusimamia na kuratibu taasisi hizo, na wajibu wa Taasisi hizo katika kutimiza matakwa ya kisheria ikiwemo ulipaji wa kodi.
“Upo umuhimu mkubwa wa kukutana na kujadili masuala yanayohusu Asasi za Kiraia katika Mkoa wetu, kwa kuwa sekta hii ni muhimu katika kuchagiza maendeleo na ustawi wa wananchi, Serikali inathamini mchango na kazi zinazofanywa na Asasi hizi kwa ajili ya manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla”
“Tunapoikuza jamii yetu ya kitanzania tunamsaidia Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kutekeleza maono yake kwenye Taifa hili na nipende kumshukuru kwani amekuwa akihamasisha tuzidi kuimarisha ushirikiano na asasi za kiraia” amesisitiza Malela
Kwa upande wake Mwakilishi wa Uratibu wa Mafunzo kutoka Taasisi ya foundation For Civil Society Rehema Malongo, amesema mafunzo hayo yalianza kutolewa mwaka 2020 baada ya sheria zinazoendesha mashirika nchini kubadilika.
Ameeleza kuwa lengo ni kuzidi kujenga uelewa juu ya sheria za nchi zinavyoelekeza, ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa kazi za asasi zisizo za kiserikali zinafanyika kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
“Tunatarajia kuwa baada ya mafunzo hayo tutakuwa tumejenga uwezo na uelewa juu ya masuala muhimu, na mategemeo ni kuwa kila asasi itaenda kufanya shughuli zake kwa kuzingatia miongozo mbalimbali ya nchi” amesema Rehema Malongo.
Akiwasilisha mada kuhusu “utaratibu wa utendaji wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali” katibu tawala msaidizi Mkoa wa Mtwara anayeshughulikia mipango na uratibu Edna Katalaiya amesema utaratibu wa uwepo wa mafunzo ya aina hii ni muhimu kwa ajili ya kukumbushana masharti, sheria na taratibu za nchi.
Ameeleza kwamba taarifa za Mashirika yasiyo ya Kiserikali zinapatikana kwa Serikali na umma kwa ajili ya matumizi, pia kuhimiza ushirikiano wa kisekta kati ya Wizara mbalimbali katika maswala yanayohusiana na NGOs (Kifungu cha 4 (1) (a) (c) na (d).
Mada nyingine iliyowasilishwa wakati wa mafunzo hayo ilihusu “Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali” iliyowasilishwa na Denis Bashaka ambaye ni wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Msajili wa Mashirika yasiyo ya kiserikali makao makuu Dodoma.
Katika uwasilishaji wake Bashaka amewasisitiza viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali kuweka wazi vyanzo vya rasilimali zinazoendesha miradi yao, matumizi yake na shughuli zinazotekelezwa.
Pia amewakumbusha kuwasilisha mikataba ya ufadhili unaozidi milioni ishirini kwa Msajili wa NGO na Hazina, pamoja na kuzingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji wa kifedha ikiwa ni pamoja na kuepuka matumizi mabaya ya fedha za ufadhili zinazotolewa.
Kwa upande wa mshiriki Balthazar Komba ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali ameeleza kuwa utaratibu wa mshirika kukumbushwa juu ya kufuata kanuni na sheria za nchi ni mzuri na utasaidia kukumbushana juu ya masuala muhimu.
Naye Mullowellah Mtenda kutoka Mtwara Paralegal Center ametoa wito wa kuzidisha uhusioano baina ya serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali na kuweke mazingira rafiki wezeshi ya kufanya kazi kwa pamoja.
“Sisi tunafanya kazi na Serikali hivyo ni wadau ambao tunatakiwa kuwa kitu kimoja ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira rafiki ya kuwezeshana kwa namna mbalimbali pale inapohitajika” Amesema Mtenda.
Washiriki wengine waliohusika katika mafunzo hayo ni Vyama vya kidini, Vyama vya wavuvi, Vyama vya wafanyabiashara, madini na kilimo, Vyama vya wafanyakazi, Vyamam vya wafanyabiashara wanawake, vyama vya wajane, na vyama vya watu waoanishi na Virusi vya Ukimwi.
Taasisi ya Foundation for Civil Society ilianzishwa mwaka 2002 na kusajiliwa rasmi 2003, ikiwa imejikita kwenye Kutoa ruzuku na mafunzo kwa mashirika yasiyo ya kiserikali Tanzania na Zanazibar.