Mwenyekiti wa Halimashauri ya Mji wa Mbulu Bw. Peter Martin Sulle, akiwa mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi kujibu tuhuma zinazomkabili. Baraza hilo linaafanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma.
…………………………………….
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu Bw. Peter Martin Sulle leoo Septemba 13, 2022 amefikishwa kwenye Baraza la Maadili kwa tuhuma za kumshambulia mtumishi mmoja wa halmashauri ya mji wa Mbulu kwa lugha zisizo na staha na kumuita mshamba.
Imedaiwa mbele ya Baraza la Maadili na Wakili wa Serikali Bi. Emma Gelani kuwa Bw. Sulle anadaiwa kutenda kosa hilo tarehe 29/7/2021 alipokuwa akiendesha kikao cha Baraza la Madiwani mjini Mbulu.
Katika lalamiko hilo Namba 6 la mwaka 2022, wwakili Emma amesema, “Bw. Peter Martin Sulle alimshambulia Bw. Joseph Laurent Geheri kwa lugha zisizo na staha kuwa ni mshamba, amechoshwa naye kwa kuwa ameshindwa kumtengenezeamagari na kumpatia gari lenye adhi yake.”
Akiwasilisha malalamiko hayo mbele ya Baraza la Maadili ya Viongoz, Wakili Emma ameeleza kuwa kitendo hicho kinamfanya Bw. Sulle ambaye ni kiongozi wa umma kwa mujibu wa kifungu cha nne cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 kushindwa kutimiza matakwa ya kifungu cha 6(1)(a) na (b), hivyo kukiuka Maadili ya Viongozi wa Umma kifungu cha 6(2) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Hata hivyo, baada ya maelezo hayo, mlalamikiwa alikili kosa.
Baada ya kukili kosa, Wakili Emma aliliambia Baraza la Maadili ya Viongozi kuwa, “Kwakuwa mlalamikiwa hakuna haja ya kuita mashahidi isipokuwa tunawakilisha vielelezo mbele ya Baraza kwa ajili ya hatua zaidi.”
Aliongeza kuwa, “tarehe 29/7/2021, kulikuwa na kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri ya Mji wa Mbulu na Bw. Sule aliendesha kikao hicho kama mwenyekiti. Katika kikao hicho pia walikuwepo waandishi wa habari kutoka Wasafi media, wakati Bw. Sule akiendelea na kikao alitumia lugha zisizo na staha dhidi ya Bw. Geheri aliyekuwa akikaimu nafasi ya usafirishaji katika halmashauri hiyo.
Aidha Baraza la maadili ya Viongozi lilielezwa kuwa baada ya kikao mlalamikiwa alifanya jitihada za kumtafuta Bw. GEheri kuomba msamaha.
“Walipokutana Bw. Geheri alimtaka mlalamikiwa afute maneno yake na awaite Wasafi Media na kuomba radhi.”
Kwa mujibu wa Wakili wa Serikali, mlalamikiwa pia alimuomba Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mji na wazee ili wawapatanishe, hata hivyo Bw. Geheri aliendelea kusisitiza kuwa mlalamikiwa afute maneno yaliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii takwa ambalo mpaka leo bado halijatekelezwa.
Baada ya maelezo hayo mlalamikiwa aliliambia Baraza la maadili ya Viongozi kuwa, “Nakiri kuwa maelezo yaliyotolewa mbele ya baraza ni ya kweli. Sina la kupinga kutokana na maelezo yaliyotolewa kwasababu nilifanya makosa katika mazingira yaliyoelezwa.”
Aidha alilieleza Baraza kuwa alifanya kitendo ohicho kutokana na ghadhabu alizozipata kama binadamu.
“Mhe. Mwenyekiti nilighadhabika kama binadamu kwasababu tangu nilipoapishwa mwezi Desemba, 2020 katika vikao vilivyofanyika kila mwezi hadi siku ya tukio, taarifa ya bw. Geheri ilikuwa inasema kuwa manunuzi ya matengenezo ya gali yanaendelea hadi nikashindwa kushiriki katika ziara ambayo Mhe. Waziri Mkuu Kassim majaliwa aliifanya Mererani, wilayani Simanjiro mkoani Manyara.”
Hata hivyo nilisha fanya juhudi kubwa kuleta amani na kuomba tukutane na kumuomba radhi bila mafanikio.
Baada ya maelezo hayo maelezo hayo, upande wa mashtaka haukuwa na pingamizi isipokuwa uliliomba Baraza la Maadili ya Viongozi kupokea vielelezo vya taarifa ya uchunguzi wa lalamiko hilo.