Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango (wapili kulia) akizindua jengo la kutolea huduma za Saratani katika Hospital ya Rufaa ya Kanda Bugando Jijini Mwanza.
Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango akizungumza mara baada ya kuzindua jengo la huduma za Saratani katika Hospital ya Rufaa ya Kanda Bugando.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando dkt.Fabian Massaga akizungumza wakati wa kutoa taarifa ya mradi wa Jengo la Saratani lililozinduliwa leo
Muonekano wa jengo la huduma za Saratani lililozinduliwa leo na Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philp Mpango
************************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Dkt. Philip Mpango amezindua jengo la huduma za Saratani katika Hospital ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC) Jijini Mwanza.
Akizungumza mara baada ya kukagua na kuzindua jengo hilo Dkt. Mpango amesema, hapa nchini Takwimu zinaonyesha watu elfu 42 hupata ugonjwa wa Saratani kila mwaka kutokana na idadi hiyo Serikali imeamua kuongeza mapambano dhidi ya ugonjwa huo na mengine yasiyoambukiza.
“Serikali imewekeza katika kutengeneza hafua mbalimbali za kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza,na miongoni mwa mikakati iliyopo ni pamoja na kupunguza vihatarishi vya magonjwa haya kwakuelimisha jamii kuchukua hatua stahki za kuboresha mtindo wa maisha kwa kuzingatia ulaji unaofaa, kupunguza matumizi pombe kuacha matumizi ya tumbaku na kufanya mazoezi”,amesema Dkt.Mpango
Dk mpango amesema pamoja na kukamilika kwa jengo kunabaadhi ya huduma hazitaweza kutolewa kwa sasa kutokana na upungufu wa mashine za mionzi.
“Natoa maelekezo kwa Waziri wa Afya kwa mwaka huu wa fedha kupitia fedha za Global Fund kutoa bilioni 3.1 kwaajili ya ununuzi wa mashine moja ya mionzi”,amesema Dk.Mpango
Dkt. Mpango ameeleza kuwa moja ya mambo yanayosemwa kusababisha Kansa katika ukanda wa ziwa ni pamoja na kutumia maji ya kuoshea maiti na klolofomu kuhifadhi samaki, hivyo ameviomba vyombo vya udhibiti kudhibiti jambo hilo huku akiwaomba Wananchi kuacha tabia hiyo.
Kwaupande wake Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando Dkt. Fabiani Massaga, amesema ujenzi wa Mradi huo ulianza Septemba 1,2020 na umegharimu bilioni 5.6
Amesema kati ya fedha hizo bilioni 1.9 zilitoka Serikali Kuu kupitia Wizara ya Afya,bilioni 3.1 ni mchango wa hospital kupitia mapato ya ndani, wafanyakazi wa hospital pia walichangia milioni 250 pamoja na wadau mbalimbali walichangia million 400.
Amesema ukubwa wa jengo hilo ni Mita za mraba 4100 na lina ghorofa tatu
Akizitaja faida za mradi huo Dkt.Massaga amesema utasaidia kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa watakaopata huduma,utapunguza vifo vitokanavyo na Saratani,kuongezeka kwa ubora wa huduma pamoja na kupunguza gharama za maradhi kwa wagonjwa hao.
Naye Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza na Mwenyekiti wa Bodi ya Hospital ya Bugando Renatus Nkwande, amesema pamoja na Jengo hilo kukamilika bado kunachangamoto ya upungufu wa mashine mbalimbali za matibabu ya mionzi ambazo zinagharimu bilioni 14.
“Tunaiomba sana Serikali iendelee kutusaidia kupata mashine hizo hatua itakayosaidia kuboresha huduma za matibabu ya mionzi katika hosptali yetu ya Bugando sanjari na kutuunga mkono kuwapeleka kwenye mafunzo ya mionzi wataalamu wengi zaidi watakaokidhi idadi ya wagonjwa tunaowapata kwenye hospital hii”,amesema Askofu Nkwande.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima ametoa wito kwa taasisi mbalimbali za dini kuendelea kuwekeza katika Sekta ya Afya katika Mkoa huo.